Okwi atamka mambo mazuri Simba

Muktasari:

Hii ni tofauti na pale ambapo Simba na Yanga wanapokutana kwani timu moja ikifungwa mashabiki wao hufanya vurugu na wengine kupoteza maisha kabisa.

UNALIKUMBUKA lile pambano la watani la Oktoba Mosi, mwaka jana lilivyoleta kizaazaa kwa mashabiki wa Simba kung’oa viti na kuiponza timu yao kulazimika kukarabati viti zaidi ya 1700? Kisa si bao la mkono la Amissi Tambwe wa Yanga.

Sasa sikia hii kutoka hapa Uganda, ni kwamba katika Ligi Kuu ya hapa kuna mechi zaidi ya tatu ambazo ni ‘derby’ ikiwemo ile ya SC Villa dhidi ya Express lakini inasemekana hata mmoja afunge idadi kubwa ya mabao bado mashabiki hawafanyi fujo zozote kwani hawawi wengi.

Hii ni tofauti na pale ambapo Simba na Yanga wanapokutana kwani timu moja ikifungwa mashabiki wao hufanya vurugu na wengine kupoteza maisha kabisa.

Pia imeelezwa kwamba mashabiki wa soka wa Uganda hawana mapenzi na timu zao ndiyo maana mechi zikichezwa hawaingii wengi tofauti na pale inapocheza timu yao ya Taifa ambapo wanakuwa wengi na pengine uwanja kujaa.

Kocha wa SC Villa, Waswa Boswa alisema; “Huku huwezi kuona vurugu za Tanzania ama nchi nyingine timu pinzani zinapocheza, tunacheza kwa amani kabisa hata mfunge mabao mengi, Okwi akifunga napo hakuna mambo ya vurugu na wala hachukuliwi kama staa ingawa amecheza kwenye nchi kubwa.”

OKWI ATAMKA MAMBO MAZURI KWA SIMBA

Straika wa zamani wa Simba, Emmanuel Okwi alisema yupo katika harakati za kurudisha kiwango chake ili awe kwenye fomu inayokubalika.

Hivyo amewatamkia mashabiki wa Simba wanaomtamani kwamba wasubiri kwanza kiwango chake kikisharudi atatamka maneno mazuri.

Katika mchezo wa kirafiki wa kimataifa wa Uganda uliochezwa juzi Jumamosi kwenye Uwanja wa Namboole dhidi ya timu ya Jeshi la Ufaransa, Okwi alikuwa miongoni mwa wachezaji walioifungia timu hiyo mabao 3-1. Okwi alifunga bao la pili.

Okwi anayecheza SC Villa kwa sasa aliliambia Mwanaspoti; “Nimeitwa kwenye kikosi hiki baada ya kufanya vizuri kwenye timu ya Villa Jogoo, hivyo nitahakikisha nimeongeza juhudi ili niendelee kuwemo kwenye kikosi cha Taifa maana hili ndilo kusudio langu,” alisema Okwi.

Katika hatua nyingine, kipa namba moja wa SC Villa, Mrundi Arakaza Mac Arthur ameweka wazi kuwa maisha ya jijini hapa bila Emmanuel Okwi yangekuwa magumu kwake kwani hajui lugha ya Kiingereza ambayo ndiyo lugha wanayotumia jijini hapa.

“Bila Okwi sijui kama ningekuwa naambulia kitu chochote hapa maana mimi nafahamu lugha mbili tu Kiswahili na Kifaransa lugha ambazo hapa hawazifahamu. Okwi ni mtu mzuri huwa ananielekeza.”

Naye mchezaji wa timu ya Ligi Kuu Uganda ya Vipers, Erisa Sekisambu ameonyesha kukasirishwa na kitendo cha Simba kumsugulisha benchi Mganda  Juuko Murshid na kudai hilo linamkatisha tamaa kuja kucheza soka Bongo.