Nyota Mbeya City atakiwa Zambia

Friday May 19 2017

 

By Justa Musa,Mwananchi; jmusa@mwananchi.co.tz

Mbeya. Mshambuliaji wa Mbeya City, Geofrey Mlawa  yupo mbioni kujiunga na Real Nakonde ya Zambia baada ya mkataba wake kumalizika msimu huu.

Mlawa aliyesajiliwa na Mbeya City akitokea Kimondo SC amekuwa hana nafasi ya kudumu katika kikosi cha kwanza cha klabu hiyo.

Taarifa za uhakika kutoka klabu hiyo zinasema tayari mazungumzo kati ya uongozi wa Real Nakonde na Meneja wa mchezaji huyo Erik Minga ambaye ni Mkurugenzi wa Kimondo SC  yamefikia hatua nzuri.

Alipoulizwa kuhusu suala hilo Mlawa alisema anashukuru mkataba wake unamalizika msimu huu na hawezi kusaini mkataba mwinyine na Mbeya City.

"Nikaangalie maisha sehemu nyingine na hususani nje ya Tanzania ambako kabla ya kuja hapa nilipo nimecheza huku na mpira wa wenzetu mchezaji unakuwa na mengi ya kujifunza kuliko hapa kwetu,’’alisema Mlawa.

Alisema changamoto ya kutopata nafasi klabuni hapo imemfanya hata yeye kujihisi tofauti na kwamba ndiyo maana anafanya mipango hiyo ya kusakata kabumbu la nje.

‘’Mengi zaidi anayo meneja wangu na kwa sasa ni mapema mno kuweka kila kitu hadharan ila tusubiri tu pazia lifungwe hayo yote uatayapata,’’alisema.

Alipotafutwa meneja wa mchezaji huyo, Minga alijibu kwa ujumbe mfupi  kwa njia ya simu kwamba yupo safarini na suala hilo atalizungumzia mara baada ya kufungwa kwa pazia la Ligi Kuu Tanzania Bara.