Nyie Stand nyie, Mungu anawaona na misifa yenu

Waziri wa Mambo ya Ndani Mwigulu Nchemba wa Yanga (kulia) akijaribu kumtoka Mbunge William Ngeleja wa Simba katika mchezo wa kuchangia waathirika wa Tetemeko la Ardhi. PICHA | ANTHONY SIAME.

Muktasari:

  • Straika huyo alifunga bao hilo baada ya Mwinyi kuzembea kuondosha mpira

YANGA kama masihara jana Jumapili imepigwa bao, likang’ang’ania hadi dakika 90 za mchezo wao na Stand Utd zikamalizika Vijana wa Jangwani wakiwa wamelala bao 1-0 kwa Chama la Wana, kiongozi mmoja aliyeambatana na timu hiyo mkoani hapa akasikika akiwaambia Stand; ‘Mungu anawaona na misifa yenu mjue’.

Bao la dakika ya 58 la straika Pastory Athanas aliyetumia makosa ya beki wa kushoto wa Yanga, Haji Mwinyi lilitosha kuwatibulia watetezi hao wa Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) Bara rekodi yao ya kutopoteza mchezo wowote wala kuruhusu nyavu zao kuguswa msimu huu.

Straika huyo alifunga bao hilo baada ya Mwinyi kuzembea kuondosha mpira na Athanas akauwahi na kuelekea langoni na kupiga shuti lililomshinda kipa Ally  Mustafa ‘Barthez’ kwenye mchezo mkali uliochezwa kwenye Uwanja wa Kambarage.

Hicho kilikuwa kipigo cha kwanza cha Yanga na bao pekee walilofungwa Vijana hao wa Hans Pluijm, ikiwa ni siku chache tu kabla ya kuvaana na watani zao Simba ambao msimu huu wameonekana kuwa vizuri wakiongoza msimamo na pointi zao 16.

Kipigo hicho cha jana kimeiporomosha Yanga hadi nafasi ya tatu ikiipisha Stand ambayo ilikimbiwa na mdhamini wake, Kampuni ya Acacia ikiwa na pointi 12 na moja ya timu mbili pekee ambazo hazijapoteza mchezo wowote sambamba na Simba.

Katika mchezo huo wa jana, Yanga ilishindwa kufanya makeke yake kama ilivyokuwa kwenye mechi yao na Mwadui ambayo ilishinda mabao 2-0 wiki iliyopita kwani wenyeji wao walicheza jihad wakikaba mpaka vivuli vya washambuliaji wa Yanga.

Yanga itabidi wajilaumu kwa kipigo hicho kwani walipoteza nafasi nyingi za wazi hasa kipindi cha kwanza kupitia Simon Msuva, Donald Ngoma na  Amissi Tambwe kabla ya Obrey Chirwa kuingia kipindi cha pili na kutofanya lolote la maana.

Katika mechi nyingine ya ligi hiyo, Toto Africans ikiwa ugenini Mlandizi Pwani iliambulia sare isiyo na mabao mbele ya Ruvu Shooting kwenye Uwanja wa Mabatini.

NCHEMBA KAMA POGBA

Katika hatua nyingine Wabunge wanaoishabiki Yanga jana walijipoza machungu walipowalaza wenzao wa Simba mabao 5-2, huku Waziri wa Mambo ya Ndani, Mwigulu Nchemba akitupia mbili, Uwanja wa Taifa.

Mchezo huo ulikuwa maalum kuchangisha fedha kwa wahanga wa Tetemeko la Ardhi wa Mkoa wa Kagera, ambapo mabao mengine ya wabunge wa Yanga yalifungwa na Khamis Sadifa aliyefunga pia mawili na Mohammed Mchengerwa, huku mabao ya Simba yakifungwa na Cosato Chumi na  Kaizer Makame kwa penalti.