Niyonzima aaga kabisa Yanga

Sunday March 19 2017Haruna Niyonzima

Haruna Niyonzima 

By Gift Macha,LusaKA

KIUNGO mwenye vitu vingi uwanjani, Haruna Niyonzima amesema huenda huu ukawa ndiyo msimu wake wa mwisho ndani ya klabu ya Yanga kwani anatazama mbele kwenda kutafuta changamoto mpya.

Nahodha huyo msaidizi aliliambia Mwanaspoti kuwa katika maisha yake ya soka hakuwahi kucheza katika klabu moja kwa muda mrefu kama alivyofanya Yanga hivyo anafikiri sasa ni wakati wa kusonga mbele.

Niyonzima alijiunga na Yanga mwaka 2011 na amekuwa mchezaji tegemeo katika kikosi cha kwanza kwa muda wote huku pia akiwa mchezaji wa kigeni aliyecheza soka nchini kwa muda mrefu zaidi.

“Dili langu la Cyprus bado lipo na nilikuwa niondoke mwezi huu, lakini kumekuwa na mwingiliano kidogo, hata hivyo nitakwenda mwezi ujao kwenda kujaribu bahati yangu,” alisema Niyonzima ambaye ni nahodha pia wa timu ya taifa ya Rwanda, Amavubi.

“Inaweza ikawa ndiyo msimu wangu wa mwisho na Yanga. Nimecheza hapa muda na kuna wakati lazima utazame mbele. Nimefurahi kuwa sehemu ya mafanikio ya klabu na sasa natazama maisha mapya,” alisema Niyonzima ambaye mkataba wake umebakiza miezi michache kumalizika.