Ni suala la muda tu, Serengeti Boys imo

Muktasari:

Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) lilikata rufaa CAF kutaka mchezaji wa Congo-Brazzaville, Langa Percy afanyiwe vipimo vya MRI kwa madai kuwa amezidi umri wa miaka 17 jambo ambalo lilipelekea Shirikisho hilo la Afrika kuwapa Congo siku 12 kumpeleka mchezaji huyo mjini Cairo, Misri kwa ajili ya kufanyiwa vipimo hivyo.

TANZANIA huenda ikapata mchekea baada ya nafasi ya kufuzu kushiriki michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika kwa vijana chini ya miaka 17 kuendelea kuwa kubwa na sasa imebaki tu kikao cha Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF) kupitisha hukumu.

Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) lilikata rufaa CAF kutaka mchezaji wa Congo-Brazzaville, Langa Percy afanyiwe vipimo vya MRI kwa madai kuwa amezidi umri wa miaka 17 jambo ambalo lilipelekea Shirikisho hilo la Afrika kuwapa Congo siku 12 kumpeleka mchezaji huyo mjini Cairo, Misri kwa ajili ya kufanyiwa vipimo hivyo.

Hata hivyo taarifa mpya ambazo Mwanaspoti limezinasa ni kwamba huenda Congo ikapewa dhamana ya kuandaa mashindano hayo na kupata tiketi ya kufuzu kama mwenyeji huku Serengeti Boys ikipita kwa mgongo huo kwa kuwa Madagascar iliyokuwa iandae michuano hiyo imeonekana kukosa vigezo.

Ofisa Habari wa CAF, Junior Binyam aliliambia Mwanaspoti kuwa kikao kijacho cha Kamati ya Utendaji ya CAF ndicho kitakachotoa hatma ya mashindano hayo na kusema kama Tanzania imefuzu ama la.

“Sifahamu kama wameshampeleka mchezaji kwa ajili ya kufanyiwa vipimo lakini ninachofahamu ni kwamba Kamati ya Utendaji ya CAF itakapokutana mapema mwezi ujao ndipo itatoa hukumu ya hiyo kesi ili kuona ni nani ana haki ya kufuzu,” alisema Binyam.

Awali, Congo ilishindwa kumpelekea Percykwa ajili ya kufanyiwa vipimo nchini Misri kwa madai yupo katikati ya vita lakini sasa wanalazimika kufanya hivyo kabla ya keshokutwa Alhamisi vinginevyo Serengeti Boys itapewa tiketi hiyo.