Ni mechi ya hesabu nzito

Muktasari:

Juma Liuzio, straika anayechezea Simba kwa mkopo akitokea Zesco ya Zambia, alisema licha ya Yanga kukaririwa kucheza pasi ndefu ila kocha George Lwandamina, anapenda kucheza pasi ndefu, anajilinda na kushambulia.

ZIKIWA zimesalia siku 12, Simba na Yanga, kukutana kwenye mechi ya Ligi Kuu Bara mzunguko wa pili, nyota timu hizo wameaanza kusomana mbinu wakidai itawasaidia kujuana ubora na udhaifu hivyo watajua namna ya kujipanga kutimiza malengo.

Juma Liuzio, straika anayechezea Simba kwa mkopo akitokea Zesco ya Zambia, alisema licha ya Yanga kukaririwa kucheza pasi ndefu ila kocha George Lwandamina, anapenda kucheza pasi ndefu, anajilinda na kushambulia.

“Nimefundishwa na Lwandamina Zesco na bahati nzuri tumetua wote kwenye usajili wa dirisha dogo, simaanishi kumkariri ila tunapaswa kujiandaa iwe kwa pasi fupi ama ndefu ili tufikie lengo,” alisema

Naye Ibrahim Mohamed ‘Mo’ amewahi kusema mechi yao na Yanga ndiyo itakayotoa majibu ya nani bingwa msimu huu na kudai kuwa wamejipanga kuonyesha msimu huu wamekuja kivingine, wapinzani wao wasiwachukulie poa.

Naye straika wa zamani wa Yanga, Abel Mziba alisema kitendo cha timu hiyo kuifunga Ngaya FC ya Comoro, mabao 5-1 kwenye michuano ya kimataifa, kinawasaidia wachezaji na kocha kuwajenga katika kujiamini.

“Yanga wanaweza kuwa na nafasi zaidi ya kuifunga Simba kwa kuwa kikosi kimedumu pamoja muda mrefu, uwepo wa Mkwasa, Lwandamina na Pluijm, itaongeza nguvu na kukiboresha kikosi na ushindi wa 5-1 dhidi ya Ngaya FC, unaongezea kujiamini na kuwa na mbinu tofauti,” alisema.

Beki wa Yanga, Haji Mwinyi amesema kitendo cha Simba, kuruhusu kupishana pointi moja ndicho kilichowaondoa kwenye mstari wa ubingwa na kujikuta wakipoteana na kudai kwamba wapinzani wao wasubiri msimu ujao.