Ngumi wameanza kuzingua mapema

Friday May 19 2017

By MWANDISHI WETU

MASHINDANO ya Ngumi ya Afrika yanatarajiwa kuanza kati ya Mei 27 Juni 4 nchini Congo Brazzazille, lakini mpaka sasa kambi ya timu ya taifa ya Tanzania haijaanza.

Katibu Mkuu wa Shirikisho la Ngumi Tanzania (BFT) Makore Mashaga aliliambia Mwanaspoti jana Alhamisi kuwa, kambi hiyo imekwama kuanza mapema kutokana na wachezaji wanaounda timu hiyo kutopata ruksa kutoka kwa waajiri wao.

Mashaga alisema aliwaombea ruksa wachezaji hao ambao wanatokea timu za majeshi, lakini hakuna majibu yaliyotolewa mpaka sasa, jambo linalowavuruga akili kwani hata wanashindwa kumuita kocha wao kutoka Kenya kuja kuanza kazi.

“Mpaka sasa kambi imekwama kuanza, ni mchezaji mmoja ambaye sio askari ila tunaendelea kufuatilia ruksa za wachezaji ili kambi ianze kujiandaa na michuano hiyo ya Afrika na ile ya Afrika Mashariki itakayonyika Kampala, Uganda,” alisema.

Mashaga alisema matarajio yao ni kutuma wachezaji watano nchini Congo na 15 Kampala ili kuipigania Tanzania.

Timu hiyo ya taifa inaundwa na wachezaji 20, watano wakiwa ni wanawake na waliosalia ni wanaume waliopatikana kupitia michuano ya Taifa iliyomalizika mwishoni mwa mwezi uliopita.