Ngumi kurindima Dar

Muktasari:

Katibu mkuu wa shirikisho la ngumi Tanzania (BFT), Makore Mashaga alisema mashindano hayo yatafunguliwa saa nane mchana kwenye viwanja hivyo, baada ya zoezi upimaji uzito kukamilika.

Mashindano ya taifa ya ngumi yanatarajiwa kuanza leo kwenye viwanja vya Tanganyika Packers jijini huku mabondia kutoka vikosi vya majeshi ya ulinzi na usalama wakitarajiwa kutamba.

Katibu mkuu wa shirikisho la ngumi Tanzania (BFT), Makore Mashaga alisema mashindano hayo yatafunguliwa saa nane mchana kwenye viwanja hivyo, baada ya zoezi upimaji uzito kukamilika.

"Mabondia wataanza kupima uzito palepale Tanganyika Packers asubuhi saa tatu na baada ya hapo ratiba ya mashindano itatolewa rasmi tayari kwa mabondia  kuingia ulingoni mchana," alisema Mashaga.

Rais wa BFT, Mutta Lwakatare alisema kuwa mashindano hayo ndio yatakayotumika kupata timu ya taifa ya ngumi itakayoshiriki mashindano ya Afrika.

"Safari hii tunataka kutengeneza timu ya taifa ambayo itakwenda kufanya vizuri na ndio maana mashindano haya tumeyafanya mapema ili tupata muda wa kutosha wa maandalizi.

"Nina imani kuwa katika mashindano ambayo tutakwenda kuwakilisha taifa letu, safari hii tutafanya vizuri kwa kuwa tumepata wawakilishi wazuri," alisema Lwakatare.