Ngoma na Okwi hawachekani sana

Muktasari:

Kama wewe ni shabiki wa Simba usicheke kwani staa wa zamani wa timu hiyo, Emmanuel Okwi naye alicheza nchini kwa miaka mitano na kufunga hatrick moja pekee kabla ya kuuzwa na Simba kwenda nchini Denmark.

KAMA ulikuwa hufahamu ni kwamba straika wa Yanga, Donald Ngoma amecheza Ligi Kuu Bara kwa msimu mmoja na nusu sasa na kufunga mabao 24 lakini kumbe hajawahi kufunga ‘hatrick’ hata moja.

Kama wewe ni shabiki wa Simba usicheke kwani staa wa zamani wa timu hiyo, Emmanuel Okwi naye alicheza nchini kwa miaka mitano na kufunga hatrick moja pekee kabla ya kuuzwa na Simba kwenda nchini Denmark.

Straika mwenye misuli na ubavu wa maana, Elius Maguli naye hadi anakwenda kucheza soka la kulipwa nchini Oman alikuwa amefunga mabao 37 Ligi Kuu Bara lakini hakuwa amefunga hatrick hata moja.

Kwa mastaa wanaocheza ligi kuu kwasasa ni Amissi Tambwe anayeongoza kwa kufunga hatrick akiwa amefunga mara sita tofauti katika kipindi cha miaka mitatu na nusu aliyocheza soka nchini. Tambwe anafuatiwa na Ibrahim Ajib wa Simba mwenye hatrick mbili.

Straika mzawa anayelipwa ghali zaidi, John Bocco wa Azam tangu ametoka kuuguza majeraha ya goti na kurejea uwanjani mwanzoni mwa mwaka 2014 mpaka leo hajaweza kufunga hatrick yoyote hivyo kufikisha siku zaidi ya 1000 bila kufanya hivyo.

Kwenye mechi za Ligi Kuu Bara msimu huu ni staa mmoja tu, Kelvin Sabato aliyefanikiwa kufunga hatrick ambapo ilikuwa katika mechi ya Stand United na Mtibwa Sugar ambayo ilimalizika kwa sare ya mabao 3-3.

 

MAKOCHA WANENA

Kocha msaidizi wa Stand United, Athuman Bilal alisema tatizo kubwa ambalo limekuwa likiwakumba mastraika nchini ni kuridhika mapema na kukosa kiu ya kufunga tena na tena ili kuweka rekodi.

“Tatizo la kwanza ni mastraika kutokuwa na kiu ya kufunga sana, mechi inaweza kuanza vizuri na mshambuliaji akafunga mapema lakini baadaye ukaona ameridhika na kupooza,” alisema Bilal.

“Hatuwezi kuwa na ligi bora kama washambuliaji wetu hawaonyeshi uwezo wa ziada. Unaweza kuona msimu huu tangu mchezaji wetu Kelvin Sabato aliyehamia Majimaji afunge hatrick bado hakuna mchezaji mwingine aliyeweza kufanya hivyo,” alisema Bilal.

Kocha Mkongwe, Meja Mstaafu, Abdul Mingange alisema tatizo kubwa linaanzia kwa wachezaji wengi nchini kukosa misingi ya soka pamoja na uwezo binafsi wa kuwaongoza kuweza kupachika mabao mengi.

“Ili mchezaji aweze kufunga hatrick lazima awe na uwezo binafsi wa kufanya hivyo. Pili lazima awe na nidhamu pamoja na misingi ya soka,” alisema Mingange.

“Kwa upande wa wachezaji wa kigeni lazima mchezaji asajiliwe akiwa katika kiwango bora. Mchezaji kama hachezi kwenye timu ya taifa hata ya hapo Zimbabwe hatuwezi kusema ni mahiri sana,’’ alisema.

“Pia walimu wamekuwa hawawafundishi wachezaji vitu vya muhimu vya kufanya. Mchezaji lazima afundishwe namna ya kupokea pasi na kutoa pasi ya bao. Kwa wachezaji wengine mahiri wanaangushwa na nguvu ya timu,” alisema Mingange.