Ngoma, Tambwe bado kidogo

Monday March 20 2017

By GIFT MACHA, LUSAKA

KOCHA wa Zanaco, Numba Mumamba amefichua kwamba kukosekana kwa staa wa Yanga, Donald Ngoma katika mchezo wa juzi Jumamosi kuliwasaidia kupata nafasi ya kusonga mbele katika mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Yanga iliondoshwa na Zanaco juzi Jumamosi baada ya kutoka sare ya bila kufungana mjini hapa ambapo wenyeji wao walikuwa tayari wana faida ya bao la ugenini kufuatia matokeo ya sare ya bao 1-1 jijini Dar es Salaam wiki moja iliyopita.

Kutokana na Ngoma kuwa majeruhi, Yanga ililazimika kumuacha jijini Dar es Salaam ili aendelee kujitibia kitendo ambacho Mumamba alidai kwamba kiliwapa nafuu kubwa mabeki wake kwani tayari walikuwa wanaumiza kichwa namna ya kumkaba.

“Kukosekana kwa yule straika aliyeanza kwenye mchezo wa kwanza (Donald Ngoma) kumetusaidia sana. Tulikuwa tumeweka mipango mingi ya namna ya kumkaba lakini alipokosekana tulisema ni nafuu,” alisema Mumamba.

“Unaona mfano Msuva (Saimon), alicheza vizuri katika mechi ya Dar es Salaam na tukaona ni mchezaji mahiri, kwenye mchezo wa leo tuliweka mpango maalumu wa kumkaba. Licha ya kwamba alijitahidi kucheza vizuri lakini hakuwa tishio,” alieleza nyota huyo wa zamani wa Zanaco. Hata hivyo kocha huyo ameitabiria Yanga kufanya vizuri na kutinga katika hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika. Mumamba alidai kwamba Yanga ina timu nzuri na itafika mbali.