Ndanje tangulia, TFF lazima iwe makini sasa

Muktasari:

Bonny aliyekuwa mahiri katika eneo la kiungo katika klabu za Tukuyu Stars,

TASNIA ya michezo nchini kwa mara nyingine tena imepata pigo baada ya nyota wa zamani, Godfrey Bonny ‘Ndanje’ kufariki dunia usiku wa kuamkia jana.

Bonny aliyekuwa mahiri katika eneo la kiungo katika klabu za Tukuyu Stars,

Prisons, Yanga na Taifa Stars, amefariki jijini Mbeya baada ya wiki kadhaa za mateso akiwa hospitalini alipolazwa kutokana na kusumbuliwa na maradhi.

Kifo cha mwanamichezo huyo ni pigo kubwa kwa soka la Tanzania, hata kama alishaondoka kwenye mechi za ushindani, lakini mchango wake kama kocha na mzoefu wa mchezo huo bado ulikuwa ukihitajika kwa muda mrefu zaidi.Hakuna mdau wa soka ambaye hafahamu umahiri wa kiungo huyo ambaye baada ya kuachana na Yanga na kutemwa Taifa Stars aliendelea kucheza kwenye mechi za mabonanza na kuwanoa vijana ili kuwarithisha kipaji chake.Ni kweli kifo kimeumbiwa viumbe hai wakiwamo wanadamu, lakini kwa hakika kinauma na kinaumiza hasa kwa tabia yake ya kutenganisha wapendanao na wakati mwingine kuwaachia upweke, majonzi na fadhaa waliosalia duniani.

Mwanaspoti linawapa pole wafiwa hususani, familia, ndugu, jamaa na rafiki pamoja na wanamichezo kwa ujumla kwa msiba wa Bonny.

Tunaungana na wanamichezo wote kumuombea marehemu katika safari yake, lakini pia kuitakia kila la heri familia yake na kuiombea iwe na subira na

uvumilivu katika kipindi hiki kigumu cha majonzi.

Wafiwa na wanamichezo kwa ujumla lazima watambue kuwa siku zote kazi ya Mungu huwa haina makosa na waungane kila mmoja kwa nafasi yake kuyaenzi yote mazuri ambayo marehemu Bonny alifanya enzi za uhai wake.

Wakati tukimtakia Godfrey Bonny ‘Ndanje’ safari njema ya kuelekea kwenye nyumba yake ya milele kwa kumuambia ‘nenda ndanje...tangulia fundi... tutaendelea kukikumbuka kipaji chako cha soka’, Mwanaspoti pia ilitaka kutoa tahadhari ya mapema kwa Shirikisho la Soka la Tanzania (TFF).

Sio kwa TFF tu bali hata kwa viongozi wa klabu za Simba na Yanga na mashabiki wa soka kwa ujumla wakati tukielekea katika pambano la watani litakalopigwa wiki ijayo kwenye Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam.

Mwishoni mwa wiki iliyopita ndani ya nchi za Angola na Afrika Kusini kulitokea majanga na vurugu katika viwanja vya soka na kusababisha vifo vya mashabiki kadhaa na makumi kwa mamia kujeruhiwa, wengine wakiwa katika hali mbaya.

Angola kulitokea maafa ya watu 17 na maelfu kujeruhiwa baada ya kutokea vurugu kwenye Uwanja wa 4 de Janeiro, uliopo mji wa Uige, zaidi ya kilomita 300 kutoka Kaskazini mwa mji mkuu wa nchini hiyol Luanda.

Vurugu hizo zilizuka wakati wa mechi ya wenyeji Santa Rita de Cassia dhidi ya Recreativo do Libolo, ambapo mashabiki walilazimisha kuingia uwanjani na kusababisha taharuki iliyofanya watu wakanyagane na kuuana.

Aidha nchini Afrika Kusini kulitokea vurugu kubwa za mashabiki baada ya Orlando Pirates kukandikwa mabao 6-0 na Mamelodi Sundowns katika mechi

ya Ligi Kuu ya nchi hiyo (PSL).

Nini kusudio letu katika hili, ni kuitaka TFF na klabu kuwa na tahadhari kuelekea pambano hilo la Jumamosi ijayo, ikizingatiwa kuwa katika mechi ya kwanza ya watani hao iliyochezwa Oktoba 1, 2016 kulitokea vurugu kabla ya wakati wa mchezo.

Mashabiki wa klabu zote walivunja viti na kung’oa viti na kusababisha askari wa kutuliza ghasia (FFU) kutumia mabomu kutuliza vurugu hizo, kitu ambacho kwa yakini kilileta doa kwenye soka la Tanzania hususani Uwanja wa Taifa.Bahati mbaya ni kwamba matukio ya vurugu michezo sio mara ya kwanza kutokea kwenye viwanja vya soka nchini, ilishatokea Mkwakwani Tanga,

Kichangani mjini Iringa kwenye Ligi Daraja la Kwanza na kwingineko.

Ili kuliepushia taifa kuingia kwenye maafa kama hayo yaliyotokea Angola na Afrika ni lazima TFF na klabu za Simba na Yanga zisaidie kuchukua tahadhari hasa kwa mashabiki wa klabu hizo juu ya kuepukana na mihemko siku ya mechi.Hatutarajii yale ya Oktoba Mosi kurejea tena kwenye mechi hiyo ijayo, lakini ni vema pia askari wanaokuwepo uwanjani kulinda usalama kudhibiti vurugu kwa njia sahihi ili kuepusha kuchochea vurugu zaidi kama ilivyotokea katika mechi hiyo ya awali.