Nasri amtetea Wenger

SEVILLE, HISPANIA. KWENYE kikosi cha Sevilla kuna askari wa zamani wa Arsene Wenger ambaye kwa sasa ameamua kushika silaha na kusimama mbele akimtetea kocha huyo akidai kwamba kufeli kwa Arsenal si makosa yake.

Askari huyo si mwingine ni Samir Nasri, Mfaransa mwenzake aliyewahi kucheza chini yake kabla ya kuhamia Manchester City ambako kwa sasa imemtoa kwa mkopo kwenda Sevilla. Nasri anasema wachezaji wa Arsenal ndiyo wanaopaswa kubeba lawama ya kiwango kibovu cha timu hiyo na si kocha wao.

Wenger amekuwa kwenye wakati mgumu tangu kikosi chake kilipochapwa 5-1 na Bayern Munich kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya. Kipigo hicho cha Bayern kilikuwa cha tatu kwenye mechi nne za karibuni baada ya kufungwa pia Watford na Chelsea na kukifanya kikosi hicho kuachwa kwa pointi 10 kwenye Ligi Kuu England.

Nasri alisema: “Huwezi kumkosoa mtu kama Wenger, haiwezekani. Arsenal ilikuwa klabu kubwa, lakini yeye ameifanya kuwa kubwa zaidi. Nadhani watu wanapaswa kuwa wakweli, si tatizo lake Arsenal kuwa mahali walipo ni wachezaji. Wachezaji ndio waliopo uwanjani na ndiyo wanaopata matokeo. Kuna mambo mengi yanatokea Arsenal, bodi na wachezaji wanapaswa kutazamwa si Wenger peke yake.”

Nasri alicheza Arsenal ya Wenger kwa misimu mitatu kabla ya kuhamia Man City mwaka 2011.