Nani kawadanganya ngumi ni ubabe!

Monday March 20 2017

By OLIPA ASSA

BONDIA wa zamani wa ngumi za kulipwa, Ali Matumla, amesema ili mchezo huo urejeshe hadhi yake uwepo mfumo wa upatikanaji wa vijana na namna ya kuwaendeleza.

Matumla alisema; “Sio kwamba hakuna mabondia wenye vipaji, ila kinachokosekana ni ukosefu wa watu wa saikolojia na mifumo sahihi ya kuwapata kisha wakaendelezwa  ili waweze kunufaika na vipaji vyao.”

Alifafanua kuhusiana na saikolojia kwamba, vijana wakielimishwa vyema kuwa ngumi si ubabe, matendo mabaya mtaani badala yake wajue kuwa ni kazi kama ilivyo mchezo wa kikapu, wavu, kriketi na soka ndipo taswira inaweza kubadilika.

“Zamani tulikuwa tunatokea kwenye kampuni ndicho kilichokuwa kinatusaidia kujitambua kwamba, tunahitaji kuheshimu mchezo wa ngumi, kuchukulia kama tunajenga afya, inasaidia kutangaza nchi tulipokuwa tunakwenda kushiriki nje pia ilikuwa ajira,” alisema Mzee Matumla.

Alisema chama kinachosimamia mchezo huo kitaifa, kijenga utaratibu kuhakikisha hadhi ya ngumi inarudi na sio kama inavyochukuliwa wa kihuni na baadhi ya watu katika jamii.

“Wadau wengine wanaelewa kwamba ngumi ni ajira, tunayaomba makampuni yajitokeze kudhamini mchezo huo kwa kufanya hivyo, itawasaidia vijana wetu kunufaika na kuweka imani kwamba upo kama soka,” alisema.