Mzuka walionao Simba, mtu anakula nyingi Taifa

Muktasari:

  • Hapo kwenye kiungo, Jonas Mkude, Mdhamiru Yasin, Mwinyi Kazimoto, Said Ndemla, Mohammed Ibrahim wako vizuri.

ACHANA na ukweli kwamba Simba itacheza mechi sita mfululizo ndani ya Uwanja wa Taifa kabla ya kwenda mkoani. Kwa mujibu wa daktari wa Simba, Yassin Gembe ni mchezaji mmoja tu Hamad Juma mwenye majeruhi na hawezi kuonekana uwanjani leo Jumamosi.

Hiyo inamaanisha kwamba huku nyuma mabeki wote unaowajua akiwemo Mzimbabwe, Method Mwanjali, Juuko Murshid, Novati Lufungo, Mohammed Hussein Tshabalala wote wako fiti kinoma.

Hapo kwenye kiungo, Jonas Mkude, Mdhamiru Yasin, Mwinyi Kazimoto, Said Ndemla, Mohammed Ibrahim wako vizuri.

Kule mbele sasa Fredrick Blagnon Muivorycoast, Laudit Mavugo wa Burundi, Ibrahim Ajib. Huku pembeni kuna Shiza Kichuya na Jamal Mnyate.  

Simba wanacheza mechi yao ya pili ya ligi ambapo kama wataendeleza mbwembe za ushindi kama walivyofanya katika mechi ya kwanza, watajiimarisha kileleni na kuipa wakati mgumu Yanga ambayo kesho Jumapili itaanza msimu kwa kucheza na African Lyon ya Dar es Salaam.

Simba mpaka sasa inaongoza ligi ikiwa na pointi tatu na ushindi wowote mkubwa leo utaifanya Yanga kuwa na wakati mgumu kuishusha kileleni. Yanga itacheza mechi yake ya kiporo Jumatano ya wiki ijayo.

Kocha Msaidizi wa Simba, Jackson Mayanja alisema; “Tunacheza dhidi ya timu imara ya Ruvu, ina wachezaji wazuri hasa katika safu yao ya ushambuliaji. Tunatakiwa kuwa imara zaidi ili kushinda.”

Mayanja mapema mwaka huu,  aliiongoza Simba kuifunga Ruvu mabao 2-0 kabla ya kupoteza kwenye mchezo wa mwisho wa msimu kwa 2-1.

Kocha wa Ruvu, Malale Hamsini alisema; “Ndio tunaanza mechi yetu ya kwanza, wenzetu walishinda mechi ya kwanza na watakuwa na morali kubwa zaidi, watacheza kwa kujituma, ni lazima tuwe imara kuhakikisha tunawazuia.

“Kikosi changu kinaundwa na safu imara ya ushambuliaji ikiongozwa na Atupele Green, nawategemea katika mchezo wetu wa kesho (leo Jumamosi) na kama watakuwa makini tutashinda.

Nafahamu pia Ruvu imekuwa na wakati mgumu pindi inapocheza na Simba, lakini tunaweza kubadilisha upepo,” alisema kocha huyo aliyekuwa akiifundisha Ndanda ya Mtwara msimu uliopita.

Kwenye Uwanja wa Azam Complex, Azam watakuwa wenyeji wa Majimaji ya Songea. Azam inasaka ushindi wake wa kwanza baada ya kulazimishwa sare ya 1-1 na Lyon kwenye mchezo wa kwanza. Majimaji ilipoteza nyumbani dhidi ya Prisons ya Mbeya kwa bao 1-0.

MFALME AMERUDI

Mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Bara, Yanga kesho Jumapili wataanza kampeni yao ya kusaka ubingwa wa tatu mfululizo ambapo, watakuwa wenyeji wa African Lyon kwenye Uwanja wa Taifa.

Yanga inatoka kuhitimisha mechi zake za hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika ambapo imemaliza mkiani katika kundi lake ikiwa na pointi nne baada ya kushinda mchezo mmoja pekee katika michezo sita.

Kocha Msaidizi wa Lyon, Ramadhan Aluko alisema licha ya Yanga kupoteza mchezo wa mwisho dhidi ya TP Mazembe, walicheza kwa kiwango cha juu na ni ishara kuwa mchezo wa kesho utakuwa mgumu.

“Yanga sio kuwa ni wabaya kwa kuwa wamefungwa na Mazembe, hapana, walicheza vizuri na tunategemea kwenye mchezo wetu watakuwa vizuri pia, ushindani utakuwa mkubwa.

“Kwa upande wetu tumejiandaa vizuri, tuna majeruhi wachache baada ya mchezo wa kwanza dhidi ya Azam, lakini sio tatizo.

Pia tunashukuru tumepewa nafasi ya kuanza na hawa vigogo ili kuona namna tulivyojiandaa,” alisema kocha huyo wa zamani wa Coastal Union ya Tanga.