Mzambia aja na kiungo wake Yanga

George Lwandamina

Muktasari:

Mnyama akimaliza mchezo wa leo anaanza ziara ngumu ya mechi tatu za Kanda ya Ziwa. Lakini habari za uhakika za ndani kabisa ambazo Mwanaspoti inazo ni kwamba George amefikia hatua nzuri ya makubaliano na Yanga ndio maana machale yanazidi kumcheza Hans Pluijm.

SIMBA inacheza na Mbao leo Alhamisi kwenye Uwanja wa Uhuru. Taarifa ambazo huzijui ni kwamba mechi nyingine ambayo Simba watakanyaga tena katika nyasi hizo, kocha mpya wa Yanga, Mzambia George Lwandamina atakuwa jukwaa kuu akiwasoma.

Mnyama akimaliza mchezo wa leo anaanza ziara ngumu ya mechi tatu za Kanda ya Ziwa. Lakini habari za uhakika za ndani kabisa ambazo Mwanaspoti inazo ni kwamba George amefikia hatua nzuri ya makubaliano na Yanga ndio maana machale yanazidi kumcheza Hans Pluijm.

Habari za ndani zinadai kwamba George ameangalia kwa umakini mechi tatu za Yanga ikiwemo dhidi ya Simba na kumbonyeza kiungo mmoja wa Zambia kwamba akae mkao wa kula akishasaini tu Jangwani anambeba.

Lakini wachambuzi wa soka wa Tanzania wametoa maoni ambayo yanafanana na kile anachokifikiria. George anajiunga na Yanga akitokea Zesco United ya Zambia ambayo ilifika hatua ya nusu fainali ya Klabu Bingwa Afrika mwaka huu kabla ya kuondoshwa na Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini iliyotinga fainali.

Makocha Mshindo Msola, Selemani Matola na nyota wa zamani wa Yanga, Aaron Nyanda kwa pamoja wamekiri kuwa Yanga ina tatizo la kiungo mkabaji huku pia wakidai kuwa mabadiliko hayo ya benchi la ufundi yangesubiri mpaka dirisha dogo ili kuepusha migongano.

Matola ambaye ana heshima kubwa ndani ya Simba, alisema Yanga ina tatizo la kiungo mkabaji hivyo kama Mzambia huyo atachukua timu ni lazima atafute mchezaji anayeweza kumudu vizuri nafasi hiyo.

“Pluijm siyo kocha mbaya, ameisaidia Yanga kupata mafaniko ila wakati mwingine huwezi kuzuia mabadiliko, nadhani wangesubiri hadi dirisha dogo. Kwenye timu ya sasa kama atakuja kocha mpya nadhani atahitaji kuongeza nguvu katika kiungo mkabaji, eneo hilo limepungua nguvu,” alisema Matola ambaye amewahi kuwa kocha msaidizi wa Simba.

Nyanda ambaye ni miongoni mwa wachezaji wachache wasomi waliowahi kucheza Yanga na ambaye pia amewahi kuwa Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Yanga, alisema kama Lwandamina atatua ni lazima afanye maboresho katika eneo la kiungo kwa kuongeza kiungo mkabaji, kiungo mshambuliaji na beki wa pembeni anayemudu kucheza kushoto na kulia.

“Yanga ina viungo watatu tu, ni wachache sana, kama atakuja anaweza kusajili kiungo mmoja wa chini, kiungo mmoja mshambuliaji anayemudu pia kucheza kama namba 10, anaweza pia kutafuta beki wa pembeni ambaye anamudu kucheza pande zote, waliopo sasa wakiumia tunakuwa na upungufu,” alisema Nyanda ambaye aliacha mpira bado akiwa kipenzi cha mashabiki.

Msolla ambaye amewahi kuifundisha Taifa Stars alisema ni kweli Yanga kuna wakati imekuwa na upungufu katika eneo la kiungo lakini siyo lazima isajili mchezaji mpya kwani beki wao wa kati Kelvin Yondani anaweza kuimudu nafasi hiyo vizuri.

“Tatizo kubwa ni kwamba Makapu (Said Juma) hakuwa anapewa nafasi ya kucheza mara kwa mara ndiyo maana tunaona ameshuka, kwa sasa siyo lazima wasajili kiungo mpya, kuna mtu kama Yondani (Kelvin) ana sifa zote za kucheza kiungo,” alisema Msolla ambaye ndiye kocha msomi zaidi kwenye ardhi ya Tanzania.