Mwanjali ampa kiburi Omog

Monday January 9 2017Kocha wa Simba, Joseph Omog

Kocha wa Simba, Joseph Omog 

By Gift Macha,Unguja

Kocha Joseph Omog hana mchezaji staa katika kikosi chake cha wachezaji 27 na amekuwa akimpa nafasi ya kucheza kila mchezaji lakini amekutana na kiburi cha beki Mzimbabwe, Method Mwanjali.

Mapema wakati msimu unaanza, Omog aliwaambia mabosi wa Simba wamtafutie wachezaji wa kazi ambapo walisajili wachezaji karibu 10 akiwemo Mwanjali aliyejiunga na timu hiyo kama mchezaji huru.

Kama hiyo haitoshi wakati wa dirisha dogo, mabosi wa Simba walimtafutia Omog wachezaji wanne wapya lakini wote hao wameshindwa kuvunja rekodi ya Mwanjali ambaye amewahi kucheza timu mbalimbali za Afrika Kusini ikiwemo Kaizer Chiefs.

Kama ulikuwa hufahamu ni kwamba katika wachezaji wote 14 ambao wamesajiliwa na Simba msimu huu, ni Mwanjali pekee aliyeweza kucheza mechi zote 21 ambazo Simba imeshiriki katika Ligi Kuu Bara na Kombe la Mapinduzi.

Rekodi hiyo ya Mwanjali inakwenda sambamba na ile ya beki wa kushoto wa timu hiyo, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ ambaye ndiye mchezaji pekee kati ya wale waliokuwepo awali ambaye ameweza kucheza dakika zote klabuni hapo.

Kocha Msaidizi Simba, Jackson Mayanja alikiri Mwanjali amekuwa katika kiwango bora tangu amefika klabuni hapo na imekuwa vigumu kumwondoa katika kikosi cha kwanza.

“Amekuwa na kiwango bora mechi hadi mechi, anacheza vizuri kuliko wachezaji wote wa safu ya ulinzi hivyo ni vigumu kusema tumtoe na tumpe mtu mwingine nafasi,” alisema.

“Hata hivyo alisajiliwa ili acheze, hiyo ndiyo kazi yake ya msingi na anaifanya vizuri. Anajitolea kile alichokuwa nacho,’’ alisema.