Mwambusi: Yanga lazima kuivaa Everton

Muktasari:

Mwambusi aliyasema hayo wakati Yanga ikiwa Arusha kujiandaa na mechi yake ya kirafiki dhidi ya AFC kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini hapa.

Arusha: Kocha msaidizi wa Yanga, Juma Mwambusi amesema watatumia mchezo wa kesho dhidi ya AFC kama maandalizi ya mashindano ya SportPesa yanayotajiwa kuanza kufanyika Juni 5.
Mwambusi aliyasema hayo wakati Yanga ikiwa Arusha kujiandaa na mechi yake ya kirafiki dhidi ya AFC kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini hapa.
“Tumejipanga kushindana ili kuwa mabingwa wa mashindano hayo ili watu wajue sisi ndio wakimataifa hivyo kila shindano linalokuja mbele yetu tutahakikisha tunakuwa mabingwa tukianza SportPesa.”


“Tuna misimu miwili wachezaji hawajapumzika ipasavyo kutokana na kuwa na mashindano mengi ndani na nje ya nchi hivyo kuna baadhi ya wachezaji wa kikosi cha kwanza wanamajeraha na tumewapumzisha kwa sasa ili waweze kujiimalishe” alisema Mwambusi.

Aliongeza kuwa ratiba ya ligi haikuwa rafiki kwa upande wao, kutokana na TFF kuibana na wachezaji kukosa hata muda wa kupumzika ndio maana kuna wakati wachezaji wake walishindwa kucheza kwa kasi kama ilivyozoeleka.
“Wakati mwingine TFF wanapaswa waangalie ratiba kwa timu zinazoshiriki mashindano mengi kwa kuweka ratiba ambayo ni rafiki kwa maana Yanga kushiriki mashindani ya kimataifa ilikuwa inabeba jina la Tanzania na siyo kama wengi mwalivyokuwa wakitafsiri."

Wapokelewa Kifalme ArushaMabingwa wa Tanzania bara, Yanga ilipokelewa kifalme jijini Arusha na mashabiki wake waliyokuwa wanawangoja kwa hamu.
Mabingwa hao walizuiliwa na mashabiki wao nje kidogo ya jiji la Arusha wakiwa wanatokea Dodoma kwenye mwaliko wao bungeni.

Mashabiki wa timu hiyo walitaka kuona kombe la mabingwa hao likitolewa kwenye gari la wachezaji wa Yanga na kuingizwa katika gari maalumu lililoandaliwa ili kila shabiki aweze kuliona hadharani katika gari la wazi.
Nahodha wa Yanga, Nadir Haroub alilazimika kushuka kwenye gari la timu ya Yanga na kwenda kupanda na kombe hilo kwenye gari hilo la wazi na kuanza kulipitisha kwenye mitaa ya jiji la Arusha.