Mvua yafuta mechi ya United na City

Muktasari:

Mechi hiyo iliyokuwa ipigwe nchini China imeahirishwa kutokana na mvua kubwa iliyonyesha na kuufanya uwanja ujae maji.

BEIJING, CHINA. MECHI ya kirafiki ya kujiandaa na msimu kati ya mahasimu wa jiji la Manchester, Man United na Man City iliyokuwa ipigwe usiku wa kuamkia leo imeahirishwa.

Mechi hiyo iliyokuwa ipigwe nchini China imeahirishwa kutokana na mvua kubwa iliyonyesha na kuufanya uwanja ujae maji.

Uwanja wa Beijing uliokuwa utumike kwa mechi hiyo uliwafanya makocha, Jose Mourinho na Man United na Pep Guardiola wa Man City wote kutoafiki kuchezwa mwechi hiyo.

Mourinho kwa upande wake aliuelezea uwanja huo kuwa uko katika hali mbaya wakati Guardiola alisema kitu ambacho asingekipenda ni kuona wachezaji wakiumia kutokana na uwanja huo.

Baadaye viongozi wa City na United walisema kuwa waandaaji wa mechi hiyo waliamua kuiahirisha huku habari za watabiri wa hali ya hewa zikidai kwamba mvua hizo zingeendelea leo Jumatatu hali ambayo ilizifanya timu hizo kubadili viwanja vya mazoezi.

Mechi hiyo ilitajwa kuwa ni mwanzo wa vita ya soka ya makocha, Mourinho na Guardiola ambao wamekuwa na uhasama wa muda mrefu.