Mtibwa wanakomba mapato

Friday May 19 2017

By DORIS MALIYAGA

HIVI unatambua? Wachezaji wa Mtibwa Sugar wanapiga pesa ndefu bwana kila wanaposhinda mechi zao za Ligi Kuu Bara, lakini ikitokea wamefungwa inakula kwao kwa sababu hawapati kitu chochote.

Uongozi wa Mtibwa umejiwekea mikakati kwa wachezaji wake na iko hivi; timu inaposhinda wachezaji wanazoa pesa za mapato kwa asilimia 60 na kiwanda cha Sukari Mtibwa kinatoa Sh10,000 kwa kila mchezaji, wanapotoa sare wanapata asilimia 40 na wanapofungwa hawapati kitu.

Pesa hizo zinatolewa bila kujali aina mechi na kwa wachezaji huwa wanachekelea zaidi wanapokipiga na Simba, Yanga au Azam kwa sababu mpunga huzidi.

Akizungumza na Mwanaspoti, Meneja wa Mtibwa, Sidi Ibrahim, alisema: “Mtibwa ina raha yake hata wachezaji wenyewe wanatambua hilo, nawashangaa wanaosema pesa hakuna, hivi unajua kila mechi wanayoshinda wao huchukua asilimia 60 ya mapato na kiwanda kinatoa posho ya Sh10,000 kwa kila mchezaji, lakini wanapotoa sare  wanapata asilimia 40  na wakifungwa ndio hawapati kitu.”

Sidi aliongeza na kufafanua, ikitokea wafadhili wengine wakajitolea kuwapa pesa za pongezi huwa ni juu yao.