Msuva kula kichwa Yanga

Winga Saimon Msuva

Muktasari:

Taarifa kutoka ndani ya klabu ya Yanga zilidai kuwa Kocha George Lwandamina amewaambia mabosi wa Yanga kuwa tangu amekuwa akimfahamu Chirwa anamfahamu kama winga wa kulia nafasi ambayo hata hivyo Msuva amemvutia zaidi.

WINGA Saimon Msuva huenda akaondoka na mchezaji mmoja wa kigeni baada ya kubainika kuwa anamudu vizuri winga ya kulia kuliko Mzambia, Obrey Chirwa ambaye imebainika kuwa siyo straika bali ni winga.

Taarifa kutoka ndani ya klabu ya Yanga zilidai kuwa Kocha George Lwandamina amewaambia mabosi wa Yanga kuwa tangu amekuwa akimfahamu Chirwa anamfahamu kama winga wa kulia nafasi ambayo hata hivyo Msuva amemvutia zaidi.

Kwa mujibu wa taarifa hizo ni kwamba kocha huyo amependekeza kama Amissi Tambwe na Donald Ngoma wanasalia klabuni hapo ni vyema pia akaletewa straika Mzambia Winston Kalengo ili kuwaongezea nguvu lakini bado haijafahamika mara moja kama Chirwa atakatwa ama la.

“Kocha anataka straika mwingine kwani tayari amewaambia mabosi kuwa Chirwa siyo straika ni winga, anataka straika wa kati wa kuwaongezea nguvu Tambwe na Ngoma, nadhani atakuja huyo Kalengo” kilisema chanzo hicho.

“Bado majadiliano ni makubwa kwani hata Mbuyu Twite inaonekana roho inawauma kumuacha kutokana na uwezo wake wa kucheza nafasi nyingi uwanjani,” kilidokeza chanzo cha kuaminika.