Msuva ampa Sherman mechi mbili Jangwani

Saturday December 20 2014

By ELIUS KAMBILI

WINGA wa Yanga, Simon Msuva, amesema straika mpya wa timu hiyo, Kpah Sherman, ni mahiri na anaweza kuisaidia timu lakini anapaswa kupewa mechi mbili ili kuthibitisha ubora wake.

Sherman amesajiliwa na Yanga kwa mkataba wa miaka miwili akitokea Cetinkaya FC ya Cyprus na ameichezea timu hiyo mechi moja tu dhidi Simba ya Nani Mtani Jembe ambapo Yanga ililala mabao 2-0 ambapo mchezaji huyo alicheza vizuri.

Msuva alisema: “Jamaa (Sherman) ni mzuri kwani nimecheza naye mechi moja na katika mazoezi pia nimeona anafanya vizuri, huyu anaweza kutusaidia kwa kiasi kikubwa na tukafanya vizuri kama timu maana anaonekana ni mzoefu.

“Lakini siwezi kuzungumza zaidi hadi atakapocheza mechi mbili hivi angalau tunaweza kusema ana uwezo mzuri kiasi gani au ana upungufu upi, muhimu ni kutazama atafanya nini baadaye.”

Hata hivyo, Sherman ambaye ni raia wa Liberia hakuweza kumaliza mechi dhidi ya Simba wikiendi iliyopita baada ya kuumia na alipotolewa nafasi yake ikajazwa na Mrisho Ngassa.

Katika mchezo huo wa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam Sherman aliisumbua ngome ya Simba kutokana na uwezo wake wa kupiga chenga na mashuti.

Usajili wake umekuja baada ya straika, Genilson Santos ‘Jaja’ kuamua kuachana na Yanga.