Msola ajitolea bure kwa Msuva

Simon Msuva

Muktasari:

Msuva ambaye ni kinara wa mabao ligi kuu akiwa amefunga tisa sawa na Amissi Tambwe wa Yanga na Shiza Kichuya wa Simba, amekuwa kipenzi cha makocha hao na kila aliyempa nafasi amefanya vizuri.

LICHA ya mashabiki kutomwelewa winga wa Yanga, Simon Msuva amekubalika kwa makocha wote wanaoingia ndani ya kikosi hicho akiwemo, Mholanzi Hans Pluijm na Mzambia George Lwandamina na akaweka wazi siri ya mafanikio yake ni kujituma na kujitathmini kila baada ya mechi.

Msuva ambaye ni kinara wa mabao ligi kuu akiwa amefunga tisa sawa na Amissi Tambwe wa Yanga na Shiza Kichuya wa Simba, amekuwa kipenzi cha makocha hao na kila aliyempa nafasi amefanya vizuri.

Na katika kuonyesha utofauti wake na wengine ameendelea kung’ara katika mzunguko wa pili na kuwaacha waliofanya vizuri wakipoteza viwango kama ilivyowatokea, Kichuya, Mzimbabwe wa Yanga, Donaldo Ngoma na wengine.

Pamoja na Msuva kufanya vizuri, amekuwa mchezaji namba moja anayepata wakati mgumu uwanjani kwa kuzomewa na mashabiki si wa timu yake ya Yanga tu hata Watani wao Simba.

Akizungumza na Mwanaspoti, Msuva alisema: “Kwanza watu wafahamu kila kocha ana falsafa yake na ili ufanikiwe ni kuwa makini na kutekeleza anachohitaji ingawa mchezaji pia unatakiwa kuwa mjanja kuongezea vyako inapobidi pamoja na nidhamu.”

 

MSOLA AMTATHMINI KILA MECHI

Msuva mfungaji na mchezaji bora msimu wa mwaka juzi amesema, amekuwa akijitathmini na wataalamu wengine wa soka wamejitolea kumsaidia kama kocha wa zamani wa Stars, Profesa Mshindo Msola: “Nimekuwa nikifuatilia kiwango changu kila baada ya mechi, kujitathmini mwenyewe na wataalam wa soka tofauti wananisaidia.”

“Mbali na mafunzo ninayoyapata Yanga, Msola ni msaada wangu mkubwa, amejitolea kunifanyia tathmini, kila baada ya mechi ananipigia simu akitaka nimweleze nimecheza kwa kiwango gani na baada ya hapo ananihesabia makosa, ananielekeza cha kufanya na kunisifia ninapofanya vizuri,” alisema.

“Hili la mashabiki nashangaa, kila nifanyacho kwao hawakithamini, ikitokea nimekwenda nje au nimestaafu sitasahau,’’ alisema.