Mserbia wa Simba atua Dar

Dragan Popadic

Muktasari:

Mmiliki wa African Lyon, Rahim Kangezi Zamunda alisema; “Bado mazungumzo yanaendelea, hatujafikia muafaka lakini kama mambo yakienda vizuri msimu ujao African Lyon itakuwa chini ya Popadic.”

KOCHA wa zamani wa Simba, Mserbia, Dragan Popadic kumbe yupo bwana. Alikuwa kwenye klabu ya Coffee ya Ethiopia jamaa wameamua kuachana naye.

African Lyon ambayo haina presha na mashindano makubwa imeamua kumleta Bongo na miaka yake 70. Kocha huyo yuko nchini na ameanza mazungumzo na klabu hiyo na kila kitu kiko freshi sana.

Mmiliki wa African Lyon, Rahim Kangezi Zamunda alisema; “Bado mazungumzo yanaendelea, hatujafikia muafaka lakini kama mambo yakienda vizuri msimu ujao African Lyon itakuwa chini ya Popadic.”

Alisema mbali na kumleta kocha huyo, pia wanatarajia kusajili nyota kadhaa ikiwamo kutoka Cameroon.

“Timu itaanza mazoezi wakati wowote kuanzia sasa kwenye viwanja vya klabu ya Leaders, tunategemea kurejea kwenye ligi tukiwa na kasi na nguvu mpya na mipango iliyopo ni kuhakikisha Lyon inakuwa timu ya ushindani,” alisisitiza.

Lyon imerejea tena kwenye ligi baada ya kushuka na kucheza Ligi Daraja la Kwanza (FDL) msimu uliopita  ambapo inaungana na timu ya Ruvu Shooting na Mbao FC zilizopanda kucheza ligi kuu.