Mourinho ampa pole Ranieri

London, England. Kutoka kuwa mfalme wa Leicester hadi kocha wa kawaida wa Ligi Kuu England, Claudio Ranieri hatimaye amepoteza kibarua chake Alhamisi, lakini amepokea salama za pole kutoka kwa wenzake akiwamo Jose Mourinho.

Leicester hawakuonyesha nafasi yoyote ya huruma wakati walipotangaza kumtimua Ranieri aliyewapa ubingwa wa Ligi Kuu.

Ranieri na Leicester walifanya jambo kubwa katika ulimwengu wa soka wakati walipofanikiwa kunyakuwa ubingwa wa Ligi Kuu England mwezi Mei mwaka jana, lakini sasa wapo katika janga la kushuka daraja.

Japokuwa kwa sasa Jumatano iliyopita walifufua matumani yao katika Ligi ya Mabingwa walipofungwa ugenini 2-1 na Sevilla.

Kutimuliwa kwa Mtaliano huyo kuliwashangaza wengi wakiwamo makocha, wachezaji na wachambuzi pamoja na kocha wa Manchester United, Mourinho ambaye alimrithi Ranieri katika kikosi cha Chelsea mwaka 2004 ambaye alitoa pole yake kwa 'Tinkerman'.

"Bingwa wa England na Kocha bora wa mwaka wa Fifa, ametimuliwa," aliandika Mourinho katika ukurasa wake wa Instagram.

"Hayo ndiyo maisha ya soka ya sasa Claudio. Tabasamu AMICO. Hakuna wa kuifuta historia yako uliyoiandika."

Ranieri ameicha Leicester ikiwa nafasi ya 17,  pointi moja kutoka mstari wa timu za mwisho na ikijiandaa na mechi dhidi ya Liverpool itakayochezwa Jumatatu.