Mnatokaje kwa mfano!

Kocha  Mkuu wa Yanga George Lwandamina.

Muktasari:

  • Kwenye kikao chake cha ndani na viongozi ameweka wazi kwamba tatizo aliliona kwenye kiungo mkabaji na mtu wa kutupia pia ilikuwa tatizo. Hivyo akashawishi viongozi wakamuekea mezani fungu la kusajili mafundi wawili kutoka Zambia ambao ni Justine Zulu ambaye alitua nchini Jumanne alfajiri na Winston Kalengo ambaye mazungumzo yamefikia patamu.

KOCHA Mkuu wa Yanga George Lwandamina ameangalia mikanda ya mechi za Yanga mara kibao na kugundua kwamba walikuwa wana matatizo mawili makubwa ambayo amewaambia viongozi kwamba akiwapata mafundi wawili tu biashara imeisha.

Kwenye kikao chake cha ndani na viongozi ameweka wazi kwamba tatizo aliliona kwenye kiungo mkabaji na mtu wa kutupia pia ilikuwa tatizo. Hivyo akashawishi viongozi wakamuekea mezani fungu la kusajili mafundi wawili kutoka Zambia ambao ni Justine Zulu ambaye alitua nchini Jumanne alfajiri na Winston Kalengo ambaye mazungumzo yamefikia patamu.

Kocha huyo anaamini kwamba kama jamaa wakisaini wote wawili Yanga itacheza mpira mkubwa ambao haujawahi kutokea Yanga katika miaka ya hivi karibuni. Lakini wataalam wa ufundi kutoka Zambia wamemtathmini Kalengo kama mtu hatari ndani ya boksi.

Kalengo ambaye anamaliza mkataba wake na AC Leopards ya Congo Brazzaville anasifika kwa kuwalazimisha na kuwaburuza mabeki kwenye eneo la hatari na mwenye mwili mkubwa ambapo endapo Lwandamina atakuwa akimchagua kucheza kama mshambuliaji mmoja juu anaweza kutengeneza matokeo kwa haraka kama anavyofanya nchini Brazzaville.

Silaha ya pili ambayo Kalengo ambaye kabla ya kuitumikia AC Leopards msimu uliopita alitokea Zesco pia ana ujuzi wa kufunga kwa kichwa na ndio maana Wakongo wanataka kumlipa mshahara wa Dola 10,000 (Sh 21 milioni) ili asiondoke.

Itakuwa ngumu zaidi endapo Lwandamina ataamua Kalengo acheze sambamba na washambuliaji atakaowakuta Amissi Tambwe na Donald Ngoma kwani timu itakuwa na kasi ya aina yake kwenye mashambulizi.

Wakati Obrey Chirwa anatua Yanga alikuwa na makosa mengi ya kushindwa kufunga akiwa uso kwa uso na golikipa lakini video mbalimbali zinaonyesha hilo kwa Kalengo halipo. Endapo Yanga ikifanikiwa kumsainisha Kalengo atakutana na Zulu waliyecheza naye msimu wa 2013 mpaka 2015. Zulu alitarajiwa kusaini mkataba wa mwaka mmoja na Yanga jana Jumatano jioni.

Akiwa na Lwandamina, Kalengo alitupia mabao 38 kwa kutumia pasi za Zulu ambaye anamjulia aina ya pasi ndefu na zile za kupenyeza anazotaka ambazo pia Yanga zinaweza kutumiwa na Simon Msuva, Donald Ngoma na hata Tambwe.

Ingawa Yanga wamekuwa wakifanya siri kuhusiana na ishu ya Kalengo, lakini Mwanaspoti linajua lazima aje Dar es Salaam kwavile tayari wanataka kuwachomoa Vincent Bossou na Mbuyu Twite kwenye usajili. Twite anaachwa kwavile mkataba wake unalizika mwezi huu huku Bossou akiomba kununua mkataba wake aende Vietnam ambako amepewa mchongo na Emanuel Adebayor.