Mmesikia mkwara mzito wa Machaku wa Lipuli lakini?

Monday February 13 2017

By MWANAHIBA RICHARD

WINGA wa Lipuli FC, Salum Machaku ameweka wazi kwamba timu yao itafanya vizuri msimu ujao wa ligi kuu ilimradi tu wadau wajitokeze kuidhamini na kuisapoti huku akidokeza kuwa huwa hana hofu anapoondoka kikosini kwani anajua anachofanya.

Akizungumza na Mwanaspoti, Machaku anayeitumikia timu hiyo kwa misimu miwili sasa, alisema mara zote anapoondoka kwenye timu fulani huwa anaamini kwamba atapata timu nyingine kwani uwezo wa kucheza anao tofauti na watu wanavyomfikiria.

“Hatutaki timu ipande icheze msimu mmoja kisha ishuke, kitakachosaidia timu iendelee kuwepo katika ligi ni wadau kujitokeza kutoa udhamini na misaada mbalimbali itakayowapa morali wachezaji, hiyo pekee ndio dawa ya Lipuli kubaki ligi kuu kwa miaka mingi maana ina wachezaji wazuri.

“Ni kweli nimecheza timu nyingi na kuondoka. Binafsi huwa sina woga wa kuondoka kwenye timu maana najiamini kwamba najua kucheza na nina uwezo huo, hivyo ninapoondoka napata timu nyingine na ninacheza kwa mafanikio, ila bado sijafikiri kama hapa nitaondoka nasubiri mipango yao maana timu inapopanda wenye timu wanakuwa na mipango mipya,” alisema Machaku.

Machaku aliwataka wachezaji kutokuwa na woga wa maisha ya soka kwa kwenda kucheza sehemu yoyote kwa kile alichokieleza kuwa kipaji cha mtu kinalindwa kwa kucheza na si kukaa jukwaani.

“Mchezaji unapaswa kujiandaa kisaikolojia wakati wowote, maana mwenye timu anaweza kuwa na mawazo tofauti na unayoyafikiria kwamba utaendelea kuwepo hapo wakati mmiliki hahitaji huduma yako. Hata hapa nimejiandaa kisaikolojia muda ukifika basi sitakuwa na budi kuondoka kama wao watafanya mabadiliko yao,” alisema winga huyo wa zamani wa Simba, Mtibwa Sugar na Polisi Moro.