Mkude ashtukia janja ya Kamusoko

KAMUSOKO

Muktasari:

  • Mkude alisema ni kweli Simba haijazoea kupiga pasi ndefu kutokea katikati kama wanavyofanya Yanga lakini kutokana na kasi ya washambuliaji wao wa pembeni, Shiza Kichuya na Jamal Mnyate sasa anaweza kuwa anafanya utundu huo.

KIUNGO wa Simba, Jonas Mkude ameshtukia janja ya kiungo wa Yanga, Thaban Kamusoko ambaye hutumia faida ya kasi ya washambuliaji wake wa pembeni kupiga pasi ndefu ambazo zimekuwa zikiipa timu yake mabao kupitia kwa Saimon Msuva au Deus Kaseke.

Katika mchezo wa juzi Jumamosi, Mkude alipiga pasi ndefu kwa Shiza Kichuya ambaye aliitoka kirahisi safu ya ulinzi ya Majimaji na kumpiga chenga kipa Aman Simba na kufunga jepesi.

Mkude alisema ni kweli Simba haijazoea kupiga pasi ndefu kutokea katikati kama wanavyofanya Yanga lakini kutokana na kasi ya washambuliaji wao wa pembeni, Shiza Kichuya na Jamal Mnyate sasa anaweza kuwa anafanya utundu huo.

“Soka ni mchezo wa nafasi, nilimtazama Kichuya na kuona amekaa vizuri hivyo nikapiga tu moja kwa moja na unaona alikwenda kufunga,” alisema Mkude baada ya mchezo huo.

“Ni kweli kwa sasa washambuliaji wetu wa pembeni wana uwezo mkubwa hivyo kuna wakati tutacheza soka letu la pasi nyingi na kama watakuwa na nafasi nzuri tutakuwa pia tukitumia mipira mirefu,” aliongeza Mkude.

KICHUYA NAYE

Shiza Kichuya ameibuka na staili mpya ya kushangilia akiwaiga maafande wa jeshi wanavyopiga saluti na kusisitiza ndivyo atakavyowaibukia Yanga kitakapoeleweka.

Kichuya ambaye anaongoza safu hiyo ya mabao baada ya kufikisha manne idadi ambayo ni kabla ya mchezo wa jana wa Yanga na Stand United na amewaacha nyuma wengine wenye mabao matatu; Mrundi wa Yanga, Amissi Tambwe, John Bocco wa Azam,   Mrundi wa Simba, Laudit Mavugo, Rafael Daud  wa Mbeya City,  Hood Mayanja wa African Lyon, Rashid Mandawa wa Mtibwa na Abdulrahman Mussa  wa Ruvu Shooting.

Aliitambulisha staili hiyo katika mchezo wao na Majimaji walioshinda 4-0 na akasema: “Hiyo ndiyo staili yangu mpya ya kushangilia na kila nitakapofunga nitaitumia si unajua kama askari jeshini. Hii ndiyo mwanzo mwisho, hata nikitupia kwenye mechi yetu na Yanga, mambo yatakuwa hivyo.”

Licha ya kufunga mabao mawili katika mchezo huo,  hamu ya Kichuya ilikuwa kupachika matatu amalize na hat trick, lakini ameweka nadhiri ya kujitolea kwa hali na mali kuhakikisha anafanikiwa.

“Nataka matatu (alisema Kichuya huku akikimbia kushangilia bao lake).” Na baadaye mpira ulivyomalizika bila kukamilisha idadi hiyo, alisema yeye ni kijana atapambana kwa nguvu zote kwa ajili ya Simba kuhakikisha inafanya vizuri.

Naye kocha mkuu wa kikosi hicho, Mcameroon  Joseph Omog amemsifu, Kichuya na kusema ni mfano kwa sababu anapambana bila kukata tamaa: “Kichuya ni mfano Simba hata hivyo, mbali na kufanya kwake vizuri, nataka afanye vizuri zaidi.”