Mkopi majanga, Mbeya City yajipanga

Straika  mpya wa Mbeya City, Mohammed Mkopi.Picha kwa hisani ya Bin Zubeiry sport

Muktasari:

  • Mkopi aliyeichezea Prisons-Mbeya katika ligi iliyopita na kuifungia mabao matano atazikosa mechi hizo kutokana na kusumbuliwa na maumivu ya kifundo cha mguu wa kulia tatizo alililokuwa nalo tangu mwishoni mwa msimu wa 2015-2016.

STRAIKA mpya wa Mbeya City, Mohammed Mkopi aliyesajiliwa msimu huu kutoka Prisons-Mbeya atazikosa mechi zote tatu za awali za timu yake ikiwa Kanda ya Ziwa.

Mkopi aliyeichezea Prisons-Mbeya katika ligi iliyopita na kuifungia mabao matano atazikosa mechi hizo kutokana na kusumbuliwa na maumivu ya kifundo cha mguu wa kulia tatizo alililokuwa nalo tangu mwishoni mwa msimu wa 2015-2016.

Mbeya City itaanzia mechi zake za msimu huu ugenini kwa kucheza na Kagera Sugar Jumapili hii, kisha kuvaana na Toto African na Mbao jijini Mwanza kati ya Agosti 28 na Septemba 3.

Daktari wa City, Joshua Kasekwa alisema jana Jumatano kuwa, Mkopi licha ya hali yake kuimarika hataweza kucheza mechi tatu za mwanzo kwani anahitaji zaidi kufanyishwa mazoezi mepesi ya viungo.

Mchezaji huyo aliumia kabla ya mechi ya mwisho ya kigi kuu ambayo Pisons ilimaliza nafasi ya nne ikiwa na pointi 51 ikiipiku Mtibwa Sugar iliyokuwa na pointi 50.

Dk Kasekwa alisema tangu atue City, Mkopi amekuwa akishiriki mazoezi ya kawaida na wenzake lakini hakuruhusiwa kucheza mechi yoyote za maandalizi ya msimu.

“Anaweza kucheza vizuri kwa hali aliyonayo ila tutakuwa tunamuumiza zaidi. Bado anahitaji muda na mazoezi maalumu. Ndio maana nasema atakosa mechi hata tatu za mwanzo,” alisema Kasekwa.

Kwa upande wake, Mkopi alisema anaushukuru uongozi wa City kumchukua na kuanza kumsaidia kupata matibabu hadi kufikia hatua ya kuimarika na sasa anajiona yupo ‘fiti’ kucheza mechi japo anasikiliza maelekezo ya daktari.