Miembeni wala hawafikirii kusajili

Beki wa Miembeni Salum Seif, (nyuma) akionesha ukakamavu kwa kuchuana na mshambuliaji wa timu ya Malindi, Khamis Ali wakati timu zao zilipokutana Uwanja wa Amaan katika muendelezo wa Ligi Kuu Kanda ya Unguja. Miembeni walishinda bao 1-0.

PICHA NA HAJI MTUMWA.

KOCHA wa Miembeni, Suleiman Jabir amesema kuwa hafikirii kuongeza wachezaji katika kikosi chake wakati wa usajili wa dirisha dogo linalosubiriwa kwa hamu na baadhi ya timu.

Alisema wachezaji wake wana uwezo mkubwa wa kutandaza soka la kitabuni hivyo, kwa  sasa kazi inayomkabili ni kuongeza ari na hamasa kwa kikosi chake ili kufanya vizuri zaidi katika michezo ya Ligi Kuu Zanzibar.

Jabiri alitoa kauli hiyo juzi katika Uwanja wa Amaan baada ya kumalizika kwa mechi kati yao na Malindi, ambapo walishinda 1-0.

“Kwa sasa sifikirii kuongeza hata mchezaji mmoja katika kikosi changu japo tulifanya vibaya katika michezo yetu mingi, ila kitu ninachofanya ni kuhakikisha wachezaji wanarudi katika kiwango imara cha soka ambacho ni matumaini ya mapenzi na mashabiki wetu.

“Baadhi ya mashabiki wetu walikuwa wameshakata tamaa hasa kwa kuwa tunafanya vibaya katika michezo yetu, ila kwa sasa nawaomba wasiwe na shaka kabisa na tunaahidi kuwa tumejipanga vizuri kuipaisha timu na wala haishuki daraja kabisa,” alisema.

Miembeni tayari imecheza michezo 11, minne wameshinda, mitano wamefungwa na miwili wametoka sare na wana jumla ya pointi  14 kwenye msimamo na mikakati ya kuchapa wapinzani wao na kupanda juu kwa kasi kwelikweli.