Mghana aanza vizuri

Muktasari:

  • Katika mazoezi yake ya kwanza kucheza mechi ya wenyewe kwa wenyewe juzi Alhamisi, alionyesha kiwango cha juu, alipiga mashuti ya nguvu langoni na kufunga, alikontroo na kuchezesha wenzake vizuri.
  • Alifanikiwa kuwashawishi mashabiki waliofika uwanjani siku hiyo, walimpigia makofi na kumshangilia alipofanya vizuri.

STRAIKA Mghana, Diawuo Jonhson kutoka Unit FC, ameanza vizuri katika majaribio yake na kikosi cha Simba yanayoendelea Uwanja wa Highlands mkoani Morogoro.

Katika mazoezi yake ya kwanza kucheza mechi ya wenyewe kwa wenyewe juzi Alhamisi, alionyesha kiwango cha juu, alipiga mashuti ya nguvu langoni na kufunga, alikontroo na kuchezesha wenzake vizuri.

Alifanikiwa kuwashawishi mashabiki waliofika uwanjani siku hiyo, walimpigia makofi na kumshangilia alipofanya vizuri.

Kocha wa Simba, Mcameroon Joseph Omog aliliambia Mwanaspoti: “Ameanza vizuri kama ulivyoona katika mazoezi ya kwanza hajafanya vibaya, lakini hiki bado si kipimo tosha, nahitaji kumwona zaidi mazoezini na katika mechi za kirafiki.”

VITA YA NAMBA

Kama straika aliyetoka Azam FC, Ame Ally ataungana na Simba na Diawuo pamoja na Muivory Coast Blagnon Frederick watapewa mikataba, Simba itakuwa na mastraika wa kati sita, Ibrahim Ajib, Danny Lyanga na Mussa Hassan ‘Mgosi’.

Katika nafasi hiyo kwa mfumo wa 4-2-3-1, kwa mastraika anayeweza kutumika ni mmoja au wawili kwa vile pembeni watacheza mawinga na hata namba 10, anaweza kuchezeshwa kiungo mwenye uwezo wa kupachika mabao mfano wa Awadh Juma au Peter Mwalyanzi.

Hivyo kila mmoja itamlazimu apambane ili kupata nafasi hiyo ya kuanza kikosi cha kwanza cha kocha Omog.

Tangu walipocheza mechi ya kirafiki dhidi ya Polis Morogoro wakashinda kwa mabao 6-0, Blagnon ameshindwa kufanya mazoezi na timu kwa sababu ya maumivu ya misuli ya paja na Ame bado hajajiunga, wanaopambana sasa ni Lyanga, Ajib na Mgosi ambaye pia ana uwezo wa kucheza winga.

Daktari wa Simba, Yassin Gembe amesema, maumivu aliyonayo Blagnon ni ya kawaida na anapumzishwa ili apone kabisa ili atakaporudi uwanjani awe fiti.