Mbwembwe za Manji zaitoa Simba Dar

Muktasari:

Mavugo na wachezaji wengine wote wa Simba walimfuata Kocha Joseph Omog wakamwambiaje... “Kochaee tupe siku moja tu, tumalize mishemishe zetu halafu tuingie kambini Jumamosi.” Kocha akawaambia mi freshi tu lakini ngoja nicheki na viongozi tukubaliane kabisa.

KUNA mtu mmoja anaitwa Laudit Mavugo huko Simba yeye anatupia tu. Aliwapiga Majimaji kule Songea, akaja Taifa akawaumiza Prisons na juzi tena akawapiga African Lyon. Sasa unajua nini kimetokea juzi baada ya mechi na Lyon?

Mavugo na wachezaji wengine wote wa Simba walimfuata Kocha Joseph Omog wakamwambiaje... “Kochaee tupe siku moja tu, tumalize mishemishe zetu halafu tuingie kambini Jumamosi.” Kocha akawaambia mi freshi tu lakini ngoja nicheki na viongozi tukubaliane kabisa.

Alipoinua tu simu na kutamka ishu ya kuwapa uhuru wachezaji viongozi wakamwambia ; “Ishia hapohapo...Ijumaa lazima waingie kambini Zanzibar.” Msisitizo huo wa Simba ulitoka Alhamisi jioni saa chache baada ya Mwenyekiti wa Yanga, Yusuf Manji kuachiwa kwa dhamana kwenye mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu alipopandishwa kujibu tuhuma za madai ya matumizi ya dawa za kulevya aina ya Heroin.

Awali wakati Manji akiwa ameshikiliwa kwa siku kadhaa kwenye Kituo Kikuu cha Polisi Dar es Salaam, mashabiki wa Simba walitunga nyimbo mbalimbali za kuikejeli Yanga kwamba watakiona cha moto Jumamosi ijayo Uwanja wa Taifa kwenye mechi ya watani wa jadi. Lakini juzi Alhamisi jioni baada ya Manji kuachiwa mashabiki na viongozi wa Yanga walipiga vigelegele nje ya mahakama huku wakiimba nyimbo za kejeli kwa Simba kwamba ; “Bosi amerudi mtakiona.”

Omog aliiambia Mwanaspoti kwamba baada ya mchezo wa juzi wa Kombe la FA dhidi ya Lyon wachezaji waliwasilisha ombi la kupumzika siku moja ili waondoke leo lakini kikao cha uongozi na benchi lake walikubaliana kikosi hicho kiondoke haraka jana jioni kuelekea Unguja kambini.

Habari za ndani zinadai kwamba vigogo hao wameamua kuiondoa timu ili kutunza morali ya wachezaji na kuepuka maneno ya mashabiki wa Yanga yanayoweza kuwavuruga.

“Tumeondoka tuko Unguja sasa unajua wachezaji waliomba wapumzike kwa kuziaga familia zao lakini uongozi ulisema hapana ni vyema tukaondoka haraka na tumeondoka. Unajua huu mchezo utakuwa muhimu sana sasa tumeona kuendelea kuibakiza timu hapo kuna mambo yanaweza kutuathiri katika maandalizi ya mchezo huu hilo ndiyo kubwa,”alisema Omog ambaye ni kocha pekee aliyewapa Azam taji la ligi kuu.

Kuhusu beki Method Mwanjali, Omog alisema: “Tulimpumzisha mechi na Lyon ili aweze kupona sawasawa hatuna mawazo kwamba tunaweza kumkosa, imani yangu inaniambia atacheza hakuna tatizo.”

 

MWANJALI NA BOKUNGU

Mabadiliko makubwa yanaweza kuikumba safu ya ulinzi ya Simba itakapowavaa watani zao Yanga wikiendi ijayo na safu yao mpya inaweza kuwa chini ya uongozi wa beki Mkongomani, Janvier Bokungu ingawa Omog haamini kama hilo linaweza kutokea.

Licha ya kurejea kwa Abdi Banda kwenye mchezo uliopita dhidi ya African Lyon, bado kuna wasiwasi katika safu hiyo ambapo kama mmoja wapo atapata tatizo lolote itabidi Bokungu abebe mzigo huo.

Kabla ya kuumia, Mwanjali ndiye aliyekuwa beki pekee wa kati wa Simba aliyecheza mechi zote msimu huu jambo ambalo limezua hofu juu ya kukosekana kwake lakini Simba wameshusha mzuka baada ya Bokungu kuonekana kuwa na uzoefu mkubwa na nafasi hiyo ambayo amewahi kucheza akiwa TP Mazembe ya Kongo na Esperance De Tunis ya Tunisia.

Daktari wa Simba, Yassin Gembe amewahakikishia mashabiki wa Simba kuwa Mwanjali anaweza kuiwahi Yanga na kuanzia wikiendi hii anaanza mazoezi mepesi lakini bado kuna wasiwasi kuwa anaweza asiwe fiti kwa asilimia 100.

Habari mbaya Simba ni kwamba beki wao Mganda, Juuko Murshid hajarejea nchini baada ya kujiunga na timu ya taifa ya Uganda mwishoni mwa mwaka jana huku beki wao mwingine, Abdi Banda bado hayupo fiti asilimia mia moja.

Beki wa kati asilia aliyesalia klabuni hapo Novatus Lufunga amekuwa haaminiki sana kutokana na rekodi yake msimu huu. Rekodi zinaonyesha mabao sita kati ya saba ambayo Simba imefungwa msimu huu yalifungwa Lufunga akiwa uwanjani. “Itakuwa pigo kubwa kama mabeki hao watatu watakosekana katika mechi ya watani wa jadi,” alisema beki wa zamani wa Simba na Yanga, Bakari Malima ‘Jembe Ulaya’.

“Mwanjali na Banda walikuwa katika ubora, safu yao ya ulinzi imeimarika kwa kucheza mechi nyingi pamoja, kuwakosa ni kuanza maisha mapya. Safu ya ushambuliaji Yanga ipo katika kasi kubwa, kila mmoja anajitahidi kuonyesha ana kitu cha ziada ingawa bado Simba wana faida ya kuwa na viungo wengi ambao wanazuia timu yao isishambuliwe sana,’’ alisema Malima.