Mbeya City yawalaza njaa Waganda

Muktasari:

Wachezaji wanaodaiwa fedha hizo ni pamoja na mshambuliaji Tito Okello, beki  William Otongo na winga Mayanja Hood.

Mbeya.Wachezaji watatu wa Mbeya City kutoka Uganda wamedai kulala njaa kwa siku tatu baada ya kusitishiwa huduma ya chakula kutokana na kudaiwa Sh1.2milioni katika hoteli wanayokula mjini Mbeya.

Wachezaji wanaodaiwa fedha hizo ni pamoja na mshambuliaji Tito Okello, beki  William Otongo na winga Mayanja Hood.

Wachezaji hao walisema madeni hayo yametokana na kutolipwa fedha zao za mshahara na chakula kwa miezi miwili na uongozi wa klabu ya Mbeya City.

 "Tuliingia mkataba na Mbeya City,  Desemba mosi mwaka jana tukitokea African Lion ambapo makubaliano yetu ilikuwa ni kutulipa mshahara, fedha ya chakula kila mwezi, lakini hadi sasa hatujalipwa miezi miwili,"alisema Mayanja.

 

Alisema wameamua kuzungumza na Mwananchi ili kuweza kupata msaada kwani mara nyingi wamewasiliana na viongozi wa klabu hiyo hawajapatiwa majibu hivyo wamekuwa na maisha magumu kutokana na kukosa fedha na hawajui hatma yao.

 

Alisema katika madai hayo ya chakula kila mmoja na adaiwa zaidi ya Sh 400,000 ambapo mmiliki wa hoteli hiyo amezuia kuwapa chakula kuanzia  Mei 20, mwaka huu kutokana na jinsi walivyomuaidi kuwa watalipa fedha hizo endapo nao watalipwa na klabu hiyo kitu kimekwenda tofauti.

 

"Leo tumekutana na mhasibu ambaye ndiye huwa anatoa malipo, lakini hakutujibu vizuri akasema tuende tunakotaka ndiyo maana tumekuja hapa, tunashukuru mmetupokea vizuri na kutupa hii chai mmetusaidia sana Mungu awabariki, lakini bado tunahitaji msaada wa chakula."

 

Naye Otongo alisema hawana cha kufanya kwa sasa kwani hata hati za kusafilia zipo mikononi mwa viongozi wa klabu hiyo na ligi imekwisha.

"Tunachoomba watupe nauli na hati zetu za kusaifilia tuweze kurudi  kwetu kwani hapa sisi ni wageni na hakuna mtu tunayemfahamu wa kumuomba msaada," alisema Otongo.

 

Katibu wa Klabu ya Mbeya City,  Emanuel Kimbe alipoulizwa kuhusiana na suala hilo kwa njia ya simu alisema  anawapongeza wachezaji hao kufika katika ofisi ya gazeti.

 "Kama wamefika hapo nawapongeza sana, lakini ninachojua malipo yao yanashughulikiwa ni wachezaji wengi hawajalipwa na bado hawajaondoka wanasubiri."

 Alipoulizwa kuwa anawasaidiaje kuhusu masuala ya chakula, aliwataka wachezaji hao kumfuata mhasibu kwani ndiye mwenye jukumu la kutoa fedha kwa ajili ya chakula.