Mbao: Tulistahili kuwa mabingwa FA

Muktasari:

Simba ndiyo ilikuwa ya kwanza kupata bao kupitia kwa mshambuliaji wao Fredrick Blagnon na baadaye Mbao FC walisawazisha huku Shiza Kichuya akifunga bao la ushindi kwa njia ya penalti ambayo, imelalamikiwa haikuwa halali.

WACHEZAJI, benchi la ufundi na viongozi wa Mbao FC juzi Jumamosi, walishindwa kujizuia na kujikuta wakimwaga machozi baada ya Simba kutangazwa kuwa bingwa mpya wa michuano ya Kombe la FA kwa kushinda mabao 2-1. Mechi hiyo ilichezwa Uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma.

Katika mchezo huo, ambao ulionekana kuwa mgumu kwa pande zote mbili, ulimazika kwa dakika 90 huku zote zikiwa hazijafungana na ndipo ziliongezwa dakika 30 ambazo ziliwapatia Simba ushindi huo.

Simba ndiyo ilikuwa ya kwanza kupata bao kupitia kwa mshambuliaji wao Fredrick Blagnon na baadaye Mbao FC walisawazisha huku Shiza Kichuya akifunga bao la ushindi kwa njia ya penalti ambayo, imelalamikiwa haikuwa halali.

Mwamuzi wa mchezo huo, Ahmed Kikumbo wa Dodoma aliamuru penalti hiyo baada ya mchezaji wa Mbao, Asante Kwasi kuunawa mpira huo.

Kipa wa Mbao, Benedict Haule, Kwasi pamoja na kocha wao Etienne Ndayiragije walioneka kivurugwa na matokeo hayo huku wachezaji wengine wakitoa machozi kwa madai kwamba, wamenyimwa haki hadharani.

“Mpira ulikuwa mgumu na mzuri kwani, kila upande ulicheza lakini ili umalizike na Simba kuwa mabingwa mwamuzi aliamua kutengeneza ushindi upande wao. Tunashukuru tumeonyesha kiwango chetu ambacho hata wao watakubali kuwa ubingwa wao haikuwa kazi rahisi kuupata,” alisema Haule.

Upande wa Kwasi aliliambia Mwanaspoti kuwa, “Nitarajia ubingwa huu ungekuwa wetu na asingekuwa mwamuzi kutoa penalti basi Simba wasingepata ubingwa na mpira ungemalizika kwa njia ya matuta.

“Naamini hata sisi tulikuwa bora kama wao ingawa hatukuwa na bahati ya kupata ushindi ila mpira wa Tanzania unaharibiwa na waamuzi kutokuwa makini katika kutoa maamuzi yao,” alisema Kwasi.

Kwasi, ambaye mkataba wake na Mbao umemalizika aliweka wazi kwamba, bado hajazungumza na viongozi wake juu ya kuongeza mkataba mpya na amesema yupo tayari kupokea ofa.

“Nina wakala ambaye anasimamia masuala yangu ila nipo huru kucheza popote kama tutafikia makubaliano na klabu inayohitaji huduma yangu,” alisema Kwasi.

Kocha Etienne alisema: “Kila kitu kilikuwa wazi na maamuzi kiukweli yametuumiza, nawapongeza wachezaji wangu wamejituma na ndiyo maana tulifika fainali kutokana na ubora wetu, wenzetu wamechukua ubingwa ingawa kulikuwa na mapungufu mengi katika uamuzi.”