Mavugo Mungu anakuona ujue

Muktasari:

  • Mayanja alikiri Mavugo hayupo katika kiwango bora, lakini amedai hata straika wa Yanga, Amissi Tambwe naye alishawahi kupitia nyakati kama hizo kabla ya kurudi kwenye makali yake na kuwanyima raha mabeki.

ZILE shangwe na nyimbo zilizokuwa zikiimbwa na mashabiki wa Simba kushangilia ujio wa Laudit Mavugo kwa sasa hazisisiki sana, kwa vile straika huyo ni kama amezimika hivi. Lakini, Kocha Msaidizi wa Simba, Jackson Mayanja amemkingia kifua kwelikweli.

Kocha Mayanja amesema kinachomtokea Mavugo kwa sasa ni jambo la kawaida katika soka na kwamba, muda si mrefu straika huyo akirudia fomu yake ni lazima wapinzani wa Simba wataomba po taka wasitake.

Mayanja alikiri Mavugo hayupo katika kiwango bora, lakini amedai hata straika wa Yanga, Amissi Tambwe naye alishawahi kupitia nyakati kama hizo kabla ya kurudi kwenye makali yake na kuwanyima raha mabeki.

“Siamini kama ni kutokana na presha ya mashabiki kwasababu ni mchezaji anayecheza hadi timu ya Taifa, ila hiyo ni hali ambayo inawapata wachezaji wengi, labda tukienda kucheza nje ya Dar es Salaam atafanya vizuri, kikubwa hapaswi kuiruhusu presha,” alisema.

Mbali na Mayanja pia viongozi wa Simba nao wamemkingia kifua na kutoa sababu pengine mabadiliko ya viwanja nayo yanaweza kuchangia mchezaji huyo ashindwe kufanya vizuri.

Makamu wa Rais wa klabu ya Simba, Geofrey Nyange ‘Kaburu’ aliliambia Mwanaspoti kuwa hata wao wameona jinsi mchezaji huyo alivyoshindwa kupambana hasa mechi yao iliyopita dhidi ya Majimaji ambapo, Simba ilishinda mabao 4-0. Katika mchezo huo Kocha Joseph Omog akilazimika kumtoa kipindi cha kwanza.

“Tumeona na ninadhani kocha alikuwa na sababu za kiufundi kumtoa mapema ili kujilinda kwani, Mavugo amekuwa ni mchezaji anayekamiwa na anacheza kwa hofu kuogopa kujeruhiwa.

“Unajua tunaenda kucheza mechi ngumu, tunapokutana na Yanga kunakuwa na mambo mengi, ni lazima kuwa makini na wachezaji wako hasa unaowategemea,  ndio maana kuna baadhi ya wachezaji kocha hakuwatumia  kabisa akiwamo Frederick Blagnon,” alisema Kaburu.