Mastaa wenye kasi ya kufunga Ligi Kuu England

Muktasari:

Lakini, staa huyo wa Arsenal amefunga idadi hiyo ya mabao baada ya kucheza mechi 101, jambo linalomfanya asiingie kabisa kwenye ile orodha ya wakali kumi waliotumia mechi chache kufikisha mabao 50.

SUPASTAA wa Arsenal, Alexis Sanchez, ameingia kwenye orodha ya wachezaji waliofikisha mabao 50 katika Ligi Kuu England.

Lakini, staa huyo wa Arsenal amefunga idadi hiyo ya mabao baada ya kucheza mechi 101, jambo linalomfanya asiingie kabisa kwenye ile orodha ya wakali kumi waliotumia mechi chache kufikisha mabao 50.

Sanchez hawafikii hata, Michael Owen, aliyefunga mabao 50 baada ya mechi 98, Matt Le Tissier, aliyefunga baada ya mechi 97, Les Ferdinand katika mechi 96, Teddy Sheringham katika mechi 94, Jimmy Floyd Hasselbaink katika mechi 94 na Harry Kane katika mechi 90.

Hii hapa orodha

ya mastaa 11 waliotumia mechi chache kufikisha mabao 50 kwenye ligi hiyo.

ROBBIE FOWLER, MECHI 88

Huko Anfield, walifikia kiasi cha kumfanya kuwa ni Mungu wao kutokana na kile alichokuwa akikifanya ndani ya uwanja. Suala la kufunga kwa fowadi huyo Mwingereza alipokuwa Liverpool lilikuwa si mjadala kutokana na uwezo wake wa kupasia nyavu.

Hali ya kwa majeruhi ilimtibulia mshambuliaji huyo, lakini kila alipokuwa fiti na kuingia uwanjani, Fowler, alikuwa matata kwelikweli katika kufunga mabao.

Akiwa Liverpool kwenye mechi za Ligi Kuu England, Fowler mabao yake 50 ya kwanza aliyafunga baada ya kucheza mechi 88.

IAN WRIGHT, MECHI 87

Alianza kwa makali katika kikosi cha Crystal Palace. Lakini, kipindi hicho kilikuwa hata Ligi Kuu England bado haijaanza. Wakati ligi ilipoanza tu, Ian Wright, alitimkia Arsenal, ambako hakika alikwenda kuwa mtambo wa mabao katika kikosi hicho ambacho kipindi hicho kilikuwa kikiutumia Uwanja wa Highbury.

Kwenye zama zake, Ian Wright, alikuwa akifunga kama anavyotaka na ndiyo maana hata mabao yake 50 ya mwanzo kwenye Ligi Kuu England hayakuhitaji acheze mechi nyingi baada ya kufunga idadi hiyo kufuatia mechi 87 tu.

LUIS SUAREZ, MECHI 86

Straika wa Uruguay, Luis Suarez, alikuwa kiboko na kufunga kama anavyotaka katika misimu yake miwili ya mwishoni kwenye Ligi Kuu England wakati alipokuwa na Liverpool. Kwa sasa fowadi huyo aliyewahi kuingia kwenye kashfa ya kumng’ata wenzake ndani ya uwanja, anakipiga katika kikosi cha Barcelona, ambako hakika wanavuna makali yake ya kupasia nyavu kutokana na kuunda safu matata ya ushambuliaji ‘MSN’ sambamba na Lionel Messi na Neymar.

Akiwa Liverpool, Suarez alifikisha mabao 50 kwenye Ligi Kuu England baada ya kucheza mechi 86. Mechi 44 za mwanzoni alifunga mabao 15 tu, baada ya hapo akaanza kufungulia koki ya mabao.

DIEGO COSTA, MECHI 85

Ubora wake kwenye kikosi cha Atletico Madrid ulimfanya kocha, Jose Mourinho, kuinasa sahihi yake na kumleta kwenye Ligi Kuu England kuichezea Chelsea.

Msimu huu ni wa tatu kwa fowadi huyo na mambo yake si mabaya kwa sababu ameifanya klabu kuwa na uhakika na mabao zaidi ya 20 kwa kila msimu kutoka kwake.

Staa huyo Mhispaniola mwenye asili ya Brazil, bao lake la 50 kwenye Ligi Kuu England alilifunga kwenye mechi ya ushindi wa mabao 4-2 dhidi ya Southampton, ambapo siku hiyo alifunga mara mbili. Kufunga ni jambo lisilompa shida kabisa Costa baada ya mabao 50 ya kwanza kwenye Ligi Kuu England kuyafunga katika mechi 85 tu.

THIERRY HENRY, MECHI 83

Mashabiki wa Arsenal watakwambia hawajawahi kupata mchezaji mwingine anayefahamu namna ya kufunga tangu alipoondoka staa wa Ufaransa, Thierry Henry.

Pale Arsenal, Henry, ni gwiji wa klabu hasa kutokana na huduma yake aliyotoa katika kikosi hicho chini ya kocha Arsene Wenger. Henry, ambaye awali alikuwa kiungo wa pembeni kabla ya Wenger kumbadili na kuanza kumtumia kwenye nafasi ya mshambuliaji wa kati, alionyesha uwezo wa kufunga hasa baada ya mabao yake 50 ya mwanzo kwenye Ligi Kuu England kuyafunga baada ya mechi 83 tu.

KEVIN PHILLIPS, MECHI 83

Unamkumbuka Kevin Phillips? Straika huyo alikuja kuonyesha maajabu yake akiwa na kikosi cha Sunderland, ambapo licha ya kuwa na umri mkubwa, lakini Phillips kufunga kwenye Ligi Kuu England ilikuwa kama kunywa maji vile.

Katika kikosi cha Sunderland alitengeneza kombinesheni yake matata kabisa na Niall Quinn na kumfanya awe amefikisha mabao yake 50 ndani ya mechi 83 tu jambo linalomweka kwenye orodha ya washambuliaji tishio kwenye historia ya ligi hiyo.

SERGIO AGUERO, MECHI 81

Msimu huu unapoelekea mwishoni, maisha ya straika Sergio Aguero klabuni Manchester City yamekuwa si mazuri sana. Kushindwa kuonyesha makali kumemfanya kocha, Pep Guardiola, amweke benchi mara kadhaa hasa baada ya ujio wa Mbrazili, Gabriel Jesus.

Lakini, Aguero yule wa mwanzoni kabisa kwenye Ligi Kuu England alikuwa kiboko kwa kufahamu wavu ulipo baada ya mabao yake 50 ya mwanzo kwenye ligi hiyo kuyafunga baada ya mechi 81 tu akiwa na miamba hiyo ya Etihad.

FERNANDO TORRES, MECHI 72

Kipindi hicho, Fernando Torres, alikuwa Torres kweli kweli. Kiwango chake bora kabisa kufunga mabao kilimfanya apachikwe jina la Elnino na hakika Liverpool ilimfaidi alipokuwa kwenye ubora wake kabla ya kuuzwa kwa Pauni 50 milioni kwenda Chelsea alikoenda kuharibu na kuonekana mzigo.

Torres wa Liverpool alikuwa matata kwani kwenye Ligi Kuu England alitumia mechi 72 tu kufunga mabao 50 katika ligi hiyo na kuwamo kwenye orodha ya washambuliaji tishio zaidi waliowahi kutokea Ligi Kuu England.

RUUD VAN NISTELROOY, MECHI 68

Kama kulikuwa na straika wa Kidachi aliyekuwa analifahamu vyema lilipo goli basi Ruud van Nistelrooy alikuwa mahiri zaidi. Staa huyo aliyenaswa na Sir Alex Ferguson kukichezea kikosi cha Manchester United, hakumwangusha baada ya kuanza kwa kasi katika kupasia nyavu.

Van Nistelrooy alihitaji mechi 68 tu kufunga mabao 50 katika Ligi Kuu England na hivyo kuwa mchezaji wa tatu kutumia mechi chache kufikisha idadi hiyo ya mabao.

ALAN SHEARER, MECHI 66

Kwenye Ligi Kuu England, Alan Shearer, bado ni kinara wa mabao, kwamba bado anaongoza kwa mabao 60 kuweza kufikiwa rekodi yake. Staa huyo Mwingereza wingi wa mabao yake umetokana na kasi aliyoanza nayo kwa kufunga katika ligi hiyo baada ya kutumia mechi 66 tu za kwanza kufunga mabao 50 kwenye ligi hiyo kabla ya kuendelea kuwatesa makipa hadi hapo alipostaafu akiwa na mabao 260 katika Ligi Kuu England.

ANDY COLE, MECHI 65

Straika, Andy Cole, ndiye aliyeweka rekodi kali zaidi kwenye Ligi Kuu England kutokana na kufunga mabao. Mabao yake aliyofunga akiwa na Newcastle United yalimfanya kupata dili la nguvu la kwenda kujiunga na Manchester United, ambako pia alienda kuendeleza kazi yake ya kupasia mipira wavuni. Cole alifunga kwa kasi zaidi baada ya kutumia mechi 65 tu kufikisha mabao 50 katika Ligi Kuu England.