Masogange mambo mazito

Friday February 17 2017

 

By BAKARI KIANGO

Mrembo anayetesa katika video za bongo fleva nchini, Agness Gerald ‘Masogange’anayeshikiliwa na polisi kwa tuhuma za kujihusisha na dawa za kulevya ataachiwa kwa masharti ya kuwa chini ya uangalizi wa Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam.

Hata hivyo, Kamanda wa Polisi wa kanda hiyo,Kamishna Simon Sirro jana Alhamisi alisema Masogange akiwa na watuhumiwa wengine hatimaye wamepelekwa kwa Mkemia Mkuu wa Serikali kwa ajili ya kuchukua vipimo vya damu ili kubaini kama anatumia dawa za kulevya.

Masogange aliyetamba katika video za nyimbo mbalimbali ikiwamo ya Belle 9 iliyokwenda kwa jina la Masogange, alikamatwa na polisi juzi na kushikiliwa katika Kituo Kikuu cha Polisi cha Dar es Salaam.

Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Kamishna Sirro aliwaeleza wanahabari kuwa Masogange baada ya kupata majibu hayo mwanadada huyo   atafikishwa mahakamani leo Ijumaa.

Alisema polisi inamchunguza Masogange katika maeneo matatu ambayo ni kutaka kujua kama mwanadada huyo anatumia, anauza au anasafirisha dawa za kulevya.

Hii si mara ya kwanza kwa Masogange kuingia katika tuhuma hizo, Julai 9 mwaka 2013 alinaswa nchini Afrika ya Kusini na mwenzake Melisa Edward katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Oliver Tambo akiwa na dawa zilizodaiwa za kulevya aina ya Crystal Methammphetamine zenye thamani ya Sh6.8 bilioni.

Masogange na mwenzake walikamatwa katika uwanja huo wakitokea nchini na walidakwa na Maofisa wa Mamlaka ya Mapato ya Afrika Kusini wakiwa na masanduku tisa yaliyokutwa na dawa hizo kilo 150.