Masikini Kapombe, kurejeshwa Sauzi

KAPOMBE

Muktasari:

  • Akizungumza na Mwanaspoti, Daktari wa Azam, Mwanandi Mwankemwa alisema Kapombe aliugua ghafla kiasi cha kulazimika kupumzishwa Hospitali ya Agha Khan

BEKI wa Azam Shomari Kapombe kaugua ghafla na kukimbizwa hospitali siku chache kabla timu yake haijakutana na Simba juzi Jumamosi, lakini haijajulikana kinachomsumbua na atarudishwa Afrika Kusini siku yoyote kuanzia leo.

Akizungumza na Mwanaspoti, Daktari wa Azam, Mwanandi Mwankemwa alisema Kapombe aliugua ghafla kiasi cha kulazimika kupumzishwa Hospitali ya Agha Khan na baada ya kufanyiwa vipimo bado haijajulikana kinachomsumbua.

Dk Mwankemwa ambaye ni daktari mkongwe wa tiba za wanamichezo nchini alisema hadi sasa wana wasiwasi kwamba ugonjwa wa awali uliomsumbua beki huyo msimu mmoja uliopita unaweza kuwa ndiyo tatizo linalomsumbua.

Alisema kuugua kwa Kapombe kunakuja kufuatia kumaliza dawa za awali alizopewa Afrika Kusini alikotibiwa mara ya mwisho na sasa wamekubaliana arudishwe huko ili aweze kuangaliwa upya na daktari aliyemtibu awali.

“Wote tulishtuka, tulimkimbiza hospitali na wakampumzisha siku kadhaa kabla ya jana (juzi) kumtoa,” alisema.

“Tuna hofu tatizo lililomsumbua awali limerudi, japo bado hatujaonyeshwa katika vipimo alivyopimwa, tumekubaliana tumrudishe kwa daktati wake Afrika Kusini muda wowote kuanzia Jumatatu (leo) ili amuangalie,” alisema.