Masela nusura wampofue refa

Friday April 14 2017

By JUMA MTANDA, MOROGORO

PAMBANO la nusu fainali ya michuano maalumu ya Pasaka ‘Pasaka Cup 2017’ kati ya Sultan Rangers na Waamuzi FC limeshindwa kumalizika huku mwamuzi wa pembeni, Rajab Ally, akinusurika kupewa upofu baada ya kuibuka vurugu kubwa.

Mwamuzi huyo alivamiwa, kupigwa hadi kujeruhiwa juu ya jicho na mashabiki wa Sultan wakimtuhumu kupindisha sheria kwa makusudi. Hiyo ilimfanya mwamuzi wa kati Kassim Saleh kulivunja pambano hilo zikiwa zimesalia dakika 25.

Vurugu hizo zilizotia doa michuano hiyo, zilitokea kwenye Uwanja wa Sabasaba mjini Morogoro wakati Waamuzi FC wakiongoza bao 1-0 lililofungwa na Idrisa Magosi.

Dalili za utemi wa Sultan zilianza mapema baada ya beki wa timu hiyo, Ally Gau, kumvamia mwamuzi huyo na kumpiga hatua iliyomfanya aonyeshwe kadi nyekundu dakika ya 49.

Lakini wakati mchezo ukiendelea ndipo katika dakika ya 75 mashabiki wa timu hiyo walipomvamia mshika kibendera huyo na kuanza kumtwanga makonde kabla ya vurugu hizo kutulizwa na mwanajeshi aliyeamua kuingilia kati.

Mwanajeshi hiyo alitembeza kichapo kwa vijana waliokuwa wakimshambulia mwamuzi huyo na kuwafanya mashabiki hao kutawanyika baada ya kuwatandika mkanda, ila tayari wakiwa wameshamjeruhi Rajab juu ya jicho la kushoto lililovuja damu.

Katibu Mtendaji wa Chama cha Soka Manispaa ya Morogoro (MMFA), Kafale Maharagande, amelaani kitendo hicho huku kamati ya mashindano hayo ikiiondoa Sultan na  kuipa ushindi Waamuzi FC.