Manji awajibu Simba, aipa Yanga uwanja

Yusuf Manji

Muktasari:

Kumbe bosi wa Yanga, Yusuf Manji alikuwa akizisikia kebehi hizo na kuamua kufanya jambo moja ambalo ni kama jibu kwa Wana Msimbazi, baada ya kugawa eneo lake la ardhi lililopo Kigamboni na kuipa Yanga ili ijenge uwanja baab’kubwa.

MASHABIKI wa Simba wamekuwa wakiwakebehi watani zao, Yanga kuhusu uwanja wao wa Kaunda, uliopo Jangwani, hasa baada ya kupata eneo kubwa huko Bunju ambako wameanza makeke wakitengeneza uwanjani wao wa kisasa.

Kumbe bosi wa Yanga, Yusuf Manji alikuwa akizisikia kebehi hizo na kuamua kufanya jambo moja ambalo ni kama jibu kwa Wana Msimbazi, baada ya kugawa eneo lake la ardhi lililopo Kigamboni na kuipa Yanga ili ijenge uwanja baab’kubwa.

Jana Jumatano klabu hiyo ilizindua eneo hilo itakalojenga uwanja huo huko Gezaulole, Kigamboni pembezoni mwa jijini la Dar es Salaam.

Kiwanja hicho cha Manji chenye ukubwa wa Hekta 712 kimemegwa na kukabidhiwa kwa Yanga, ambapo uzinduzi wa jiwe la msingi ulifanywa na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba na Mama Fatuma Karume.

Waziri Nchemba alisema amefurahishwa na hatua ya Manji kuonyesha usikivu na kukubali ushauri aliowahi kumpa kuachana na fikra za kujenga uwanja eneo la Jangwani na kumtaka atafute maeneo ya nje ya mji kama walivyofanya Simba waliokimbilia Bunju.

Alisema anaamini uwanja huo utakuwa machinjio ya wapinzani katika Ligi Kuu na kwamba, uwanja kujengwa Gezaulole, neno ambalo kwa kizaramo lina maana ya Njoo Muone.

Kwa upande wa Mama Karume, ambaye ni mmoja wa Wajumbe wa Bodi ya Wadhamini ya Yanga, alisema Manji ni kama ameitikia wito wa wanachama waliomlilia kwenye Mkutano Mkuu wa hivi karibuni waliotaka wajengwe uwanja wao ili kuepuka kejeli za Simba.