Mandawa: Kiatu ni cha Msuva au Abdulrahaman tu

Friday May 19 2017

MSHAMBULIAJI wa Mtibwa Sugar, Rashid Mandawa, amesema atakayemnyima usingizi  Simon Msuva wa Yanga katika kunyakua Kiatu cha Dhahabu kwa ufungaji bora wa msimu ni Abdulrahaman Mussa wa Ruvu Shooting tu ambaye amepishana naye bao moja.

Msuva ana mabao 14 na Mussa anayo 13, jambo ambalo Mandawa alilieleza kwamba ni faraja kwao kuona wazawa ndiyo waliyo na nafasi kubwa hivyo akichukua mmoja wao ni sawa.

“Kila timu imebakiza mechi moja na lolote linaweza kutokea lakini kiuhalisia ukiangalia walio na nafasi mpaka sasa ni hao wawili na usipoangalia bahati hiyo itaenda kwa Mussa wa Ruvu kwani Msuva aliumia,” alisema

Mandawa anayemiliki mabao manane sasa, alisema ni maumivu kwao inapotokea mastraika wa kigeni wanachukua kiatu cha ufungaji bora kwani inakuwa inawapunguzia thamani.

Mbali na hilo alizumgumzia mafanikio aliyoyapata ndani ya Mtibwa kwamba ni kufunga mabao manane tofauti na alipotoka Mwadui alikofunga matatu na alikuwa anasugua benchi.

“Kwa tathimini kiwango changu kimepanda, nimepata nafasi ya kucheza na pia nina hatua ya kuzisakama nyavu naamini msimu ujao itakuwa zaidi,” alisema.