Manara: Tukichukua ubingwa naoa

Muktasari:

Ila hiyo sio ishu sana, jamaa ameibuka na kutangaza atafunga ndoa ndani ya mwaka huu, lakini sherehe ya kuvisha pete ataifanya mara baada ya Simba kutwaa taji la Ligi Kuu Bara.

AFISA Habari wa Simba, Haji Manara ana utani mwingi, juzi kati aliwahi kula kiapo eti, angemuoa Wema Sepetu kama Shirikisho la Soka Tanzania,TFF, lisingepangua ratiba ya Ligi Kuu Bara, lakini sasa amemkana kisa kahamia Chadema.

Ila hiyo sio ishu sana, jamaa ameibuka na kutangaza atafunga ndoa ndani ya mwaka huu, lakini sherehe ya kuvisha pete ataifanya mara baada ya Simba kutwaa taji la Ligi Kuu Bara.

Akihojiwa na Simba TV, Manara alisema ana uhakika Simba itabeba taji msimu huu na atatumia nafasi ya kufurahia ubingwa huo kwa kufanya bonge la sherehe ya kumtambulisha mchumba wake kabla ya kufunga ndoa mwishoni mwa 2017.

Katika mahojiano hayo, Manara alikiri amemtaliki aliyekuwa mkewe, huku akiweka bayana ana watoto watatu, lakini alidai hawezi kuishi bila ya mwenza ndio maana anataka kufunga ndoa na kudai mwenza wake ajaye yupo na anampenda.

Alipoulizwa juu ya Wema Sepetu, Manara alidai iliapa vile kwa kutambua kuwa, isingewezekana ratiba ya Ligi Kuu kutobadilishwa, lakini akatania kwa kusema;

“Wema ni mwanamke mzuri...kimuonekano mzuri, lakini sasa Wema yupo Chadema.., mimi pro CCM kindakindaki, wapi na wapi, ingawa mapenzi hayana siasa, hayana chama...angalau angekuwa Chadema tangu zamani, ila kwa sasa ni ngumu, japo anabaki kuwa rafiki tangu na tunasalimiana tukikutana.”

Manara pia alifunguka kuhusu Jerry Muro, Msemaji wa Yanga aliyefungiwa na TFF na kudai anammisi kama binadamu na kumsifia kwamba alikuwa akifanya soka kuwa na hamasa kubwa...ingawa alikiri alikuwa na mapungufu yake.

“Nammisi kama mwanadamu na hasa sauti yake ya kichaga, japo nimesikia kwa sasa hayupo Yanga...sijui...kwani sijawasiliana naye siku nyingi,” alisema.

Aidha Manara alifichua kuwa yeye ni Simba damu tena lialia na kutaka watu wapuuze propaganda kwamba ni Yanga akidai hawaijui vema historia yake kwa undani namna alivyoishabikia timu hiyo tangu utoto wake.

“Ilifikia wakati Yanga walitufunga mabao 3-1 wakati tunakaa hatua chache na klabu ya Yanga, mashabiki wao walipokuwa wakirudi nilikuwa nawarushia mawe...’imagine’ hapo...naipenda Simba na huwa naumia ikuifungwa,” aliongeza msemaji huyo.