Majeruhi wainyima ubingwa Liverpool

Friday May 19 2017

 

London, England. Kocha wa Liverpool, Jurgen Klopp amesema idadi kubwa ya majeruhi klabuni hapo ndiyo chanzo cha kukosa ubingwa msimu huu.

Majeruhi hao ni Sadio Mane, Philippe Coutinho, Adam Lallana, Jordon Henderson na Joel Matip

Hata hivyo,  Klopp amesisitiza kwamba msimu ujao amejipanga kusajili wachezaji wenye ubora watakaoweza kuhilimili mashindano ya Ulaya mwakani.

Kocha huyo alisema kwamba matarajio yake msimu huu ilikuwa ni kunyakua taji la ubingwa wa Ligi Kuu, hata hivyo malengo hayajatimia.

Klopp ambaye ni raia wa Ujerumani, alisema anatambua kwamba Liverpool inahitaji mabadiliko. Alisema kipindi cha usajili atatumia muda huo kusajili vijana mahiri.

“Tunatakiwa kuwa imara msimu ujao kwa sababu timu yetu imeimarika msimu huu. Tunatakiwa kufikisha asilimia mia moja za ubora.

 “Majeruhi wote ni wachezaji muhimu kikosini wamekosa michezo mingi muhimu. Tunafikiria namna gani tutaondokana na tatizo hilo msimu ujao. Hata hivyo tumejifunza mengi kutokana na jambo hili,” alisema Klopp.