Maisha ya Stand United yamshinda Kocha Mzungu

PATRICK LIEWIG

Muktasari:

  • Acacia walivunja mkataba kutokana na migogoro ya viongozi.

NDOA ya Stand United na kocha Patrick Liewig imevunjwa rasmi baada ya uongozi wa klabu hiyo kuweka wazi kuwa hawana uwezo wa  kulipa gharama zake za mshahara, malazi na mengineyo kama alivyokuwa akifanyiwa wakati klabu ina udhamini wa kampuni ya uchimbaji madini ya Acacia.

Liewig aliingia mkataba wa miaka miwili na Stand na tayari ametumikia mwaka mmoja huku Acacia nayo ikivunja mkataba wake na Stand ikiwa imebakiza mwaka mmoja. Acacia walivunja mkataba kutokana na migogoro ya viongozi.

Liewig raia wa Ufaransa anasimamiwa na mwanasheria, Mfaransa mwenzake, Franck Nicolleau, walifikia makubaliano na uongozi wa Stand kwamba mteja wake atalipwa Dola 10,000 na si mshahara wa mwezi mmoja kama viongozi wa Stand walivyopendekeza.

Habari za ndani ambazo Mwanaspoti imezipata ni kwamba viongozi wa Stand  wameandaa mkataba wa makubaliano ya kuvunja mkataba wa Liewig unaoonyesha kwamba kocha huyo alisaini mkataba Julai 20, 2015 na Stand walipendekeza kumlipa mshahara wa mwezi mmoja jambo ambalo limekataliwa na mwanasheria wa  Liewig.

Mwanasheria huyo amedai kuwa Liewig anapaswa kulipwa pesa zake zote siku ambayo atasaini makubaliano ya kuvunja mkataba vinginevyo hatua za kisheria zitachukuliwa na sheria za kazi zinaeleza ni kulipwa mshahara wa miezi 12.

Makubaliano ya kusaini mkataba huo yalipaswa yafanyike jana Jumapili baada ya mechi yao na Yanga lakini katika maelezo ambayo Mwanaspoti imepata kocha huyo huenda akasaini makubaliano hayo leo Jumatatu au kesho Jumanne.

Katibu Mkuu Stand, Kennedy Nyangi alisema: “Kweli mpango huo upo, tangu Acacia watangaze kujitoa mambo hayajakaa sawa na hatuwezi kumudu gharama, tulikubaliana mkataba tuuvunje na kocha alikubali.”