Liuzio wala sio juju, ni tizi tu

Monday January 9 2017

 

By Thomas Ng'itu

STRAIKA Mpya wa Simba, Juma ‘Ndanda’ Liuzio amefunguka akisema kuwa, ukali wake uwanjani mbele ya mabeki wa timu pinzani ni mazoezi anayopiga bila kuchoka na wala siyo kitu kingine.

Liuzio mwenye mwili jumba unaowapa wakati mgumu wapinzani wake uwanjani alisema kuwa nguvu nyingi za miguu alizonazo na pumzi ndefu uwanjani inatokana na kupenda kwake tizi mara kwa mara.

Straika huyo aliyetua Simba kwa mkopo akitokea Zesco ya Zambia, alisema kuwa wepesi wa mwili wake uwanjani licha ya kuwa mwili jumba ni sababu anapiga tizi za nguvu iwe katika gym ama mazoezini kupata kasi aliyonayo.

“Nguvu za miguu ni asili yetu, lakini muda mwingine huwa naingia Gym, hata hivyo, napiga mazoezi mchangani kwa kukimbia na hii yote ni kutafuta pumzi, pia kuongeza nguvu, hakuna kingine,” alisema.

Alisema kuwa kama mshambuliaji anatakiwa afunge, muda mwingine kwa mashuti makali na ndiyo anayoamini ni njia sahihi, na hawezi kufanya hivyo kama hana nguvu za miguu.

“Unajua unapofanya mazoezi magumu unakuwa mzito, lakini mazoezi mepesi binafsi ni msaada mkubwa kwa mchezaji kujilainisha na ndivyo ninavyofanya,” alisema.