Lipuli yakata Usimba, Uyanga

Muktasari:

  • Masenza ametoa kauli hiyo wakati wa hafla ya kuwapokea na kuwapongeza wachezaji  wa Lipuli FC  kwa kupanda Ligi Kuu msimu huu.

Iringa. Mkuu wa mkoa wa Iringa, Amina Masenza amesema timu nyingi za soka nchini hasa za mikoani zimekuwa zikiharibiwa na ushabiki wa Simba, Yanga na Azam jambo linalokwamisha maendeleo ya mpira katika mikoa hiyo.
Masenza ametoa kauli hiyo wakati wa hafla ya kuwapokea na kuwapongeza wachezaji  wa Lipuli FC  kwa kupanda Ligi Kuu msimu huu.

“Lipuli FC ni timu ya wananchi wa Iringa na ningepende hilo lieleweke na si vinginevyo, mara nyingi timu za mikoani zimekuwa zikishindwa  kupiga hatua kutokana na kuathiriwa na ushabiki wa timu kubwa za Yanga, Simba na Azam,…mimi nisengependa hilo litokea mjini Iringa kwa Lipuli FC ,” alisema Masenza.
“Lipuli FC ndiyo timu ya wanairinga na mtu yeyote atakayeonekana akishangilia timu tofauti na Lipuli FC pindi itakapocheza iwe ugenini ama uwanja wake wa nyumbani huyo atachukuliwa kuwa ni msaliti,” alisema Masena.
Masena alionya wanasisa kutotumia jina la timu hiyo kwa lengo la kujinufaisha kisiasa akidai kitendo hicho kitachochea mgawanyiko badala ya mshikamano uliopo kwa sasa.
Katibu wa Mkuu wa Chama cha Mpira Mkoa wa Iringa, Dk Ally Ngalla alisisitiza suala la kuzuia siasa kuingizwa michezoni kwa madai kuwa zingeharibu taswira ya mkoa na kuleta mgawanyiko.
“Tunakushuru kwa hatua hatua hii tuliyofikia, pia hili la kututahadharisha na ushabiki wa Yanga na Simba pamoja na siasa michezo,” alisema Dk Ngalla.
Katibu wa Lipuli FC, Willy Chikweo amewashukuru viongozi na wadau wote wa mpira kwa ushirikiano walioonyesha hadi timu inapanda Ligi Kuu.