Kwa Simba na Yanga hii, haijawahi kutokea

Utafiti wa Mwanaspoti umebaini kuwa katika kipindi cha miaka 10 iliyopita Yanga haijawahi kukutana na watani zao Simba ikiwa imetoka kupoteza mchezo hivyo, hii itakuwa ni mara ya kwanza.

Muktasari:

  • Utafiti wa Mwanaspoti umebaini kuwa katika kipindi cha miaka 10 iliyopita Yanga haijawahi kukutana na watani zao Simba ikiwa imetoka kupoteza mchezo hivyo, hii itakuwa ni mara ya kwanza.

KUANZIA kwenye vijiwe vya kahawa, mitaani mpaka kwenye daladala gumzo na mjadala ni pambano la watani wa jadi wa soka nchini, Simba na Yanga. Kila upande unatamba kuwa Jumamosi ni lazima mmoja akae, huku Simba wakitanua mabega zaidi kwa vile chama lao lipo kileleni likiwapiga chabo wapinzani wao kwa chini.

Utamu zaidi umeongezwa na kipigo ilichopewa Yanga juzi ikiwa ugenini mjini Shinyanga, lakini sasa kama hufahamu ni kwamba siku zote rekodi huwa hazidanganyi kamwe.

Utafiti wa Mwanaspoti umebaini kuwa katika kipindi cha miaka 10 iliyopita Yanga haijawahi kukutana na watani zao Simba ikiwa imetoka kupoteza mchezo hivyo, hii itakuwa ni mara ya kwanza.

Yanga ilifungwa bao 1-0 na Stand United juzi Jumapili na kuzua hofu kwa mashabiki wa timu hiyo kuelekea kwenye mchezo wa watani wa jadi hasa baada ya Simba kuifunga Majimaji kwa mabao 4-0.

Hata hivyo, watu wa Yanga wametabasamu baada ya kugundua kuwa mapema mwaka jana, Simba nao walitoka kufungwa bao 1-0 na Stand United, ilihali wao wakiifunga JKT Ruvu hapa Dar es Salaam kwa mabao 3-1, lakini Mnyama akawakalisha kwa bao 1-0. Bao la Mganda  Emmanuel Okwi aliyemchambua kipa Ally Mustafa kama karanga.

Rekodi zinaonyesha kuwa katika kipindi cha miaka 10 Simba imewahi kuingia kwenye mchezo dhidi ya Yanga ikiwa imetoka kupoteza mara mbili tofauti. Simba iliingia uwanjani kwenye mchezo dhidi ya Yanga Aprili 2011 ikitoka kufungwa mabao 4-1 na Toto Africans jijini Mwanza na kisha kufungwa tena na Yanga bao 1-0.

Hata hivyo, Simba iliondoa nuksi hiyo mwaka jana ambapo ilitoka kufungwa bao 1-0 na Stand United, lakini ikaifunga Yanga 1-0 katika mchezo uliofuata kitu ambacho kinawapa faraja Yanga kuwa pengine Stand United watakuwa wamewapaka mafuta ya upako.

Katika kipindi hicho cha miaka 10, Simba imeifunga Yanga katika michezo mitano tofauti ambapo, ushindi wao mkubwa ni ule wa mabao 4-3 iliopata mwaka 2010 na ule wa mabao 5-0 wa Mei 6, 2012 wa kukamilishia msimu na kunogesha ubingwa wao.

Yanga kwa upande wao katika kipindi hicho imeifunga Simba mara tano pia ambapo, ni mara moja tu iliingia kwenye mchezo na watani wao ikitoka kupata matokeo ya sare na ilikuwa mwaka 2013 ilipotoka sare ya bao 1-1 na Coastal Union, lakini baadaye ikaifunga Simba kwa mabao 2-0.

Kama Yanga itakubali kipigo kutoka kwa Simba wikiendi hii, itakuwa ni mara ya kwanza kwa timu hiyo ya Jangwani kufungwa mechi mbili mfululizo za Ligi Kuu tangu mwezi Mei mwaka jana. Punde baada ya kutwaa ubingwa msimu wa 2014/15, Yanga ilipoteza mechi mbili za mwisho dhidi ya Azam na Ndanda FC.