Kwa Mkude yoyote freshi tu

Monday January 9 2017Jonas Mkude

Jonas Mkude 

By Thomas Sebastian

SIMBA jana jioni ilitarajiwa kushuka uwanjani katika mechi yao ya kuwania kucheza nusu fainali ya Kombe la Mapinduzi, lakini nahodha wake mapema alisema timu yoyote watakaokutana nao iwe Yanga ama Azam kwao freshi tu.

Azam iliifanyizia Yanga kwa kuichapa mabao 4-0 katika mechi yao ya kufungia Kundi B na kushika nafasi ya kwanza na vibonde wao kukamata nafasi ya pili kwa tofauti na pointi moja na yoyote ilikuwa na nafasi ya kuvaana na Simba.

Mechi za nusu fainali zinatarajiwa kuchezwa kesho Jumanne ili kusaka timu mbili za kucheza fainali itakayopigwa Januari 13 kwenye Uwanja wa Amaan, visiwani Zanzibar kufungia msimu wa 11 wa michuano hiyo maarufu kwa sasa.

Akizungumza na Mwanaspoti, Mkude alisema timu yao haina hofu na timu yoyote na kwamba watakaoingia anga zao wahesabu maumivu kwa vile msimu huu wamejipanga kweli kweli na wapo tayari kwa mapambano.

“Soka ni mchezo wa kushindana, hivyo hata kama tukikutana na Yanga ama Azam katika hatua yoyote kwetu freshi kwa sababu tunajiamini tupo vizuri, ila muhimu ni kuona kwanza Simba inatinga nusu fainali,” alisema Mkude.

Simba ilikuwa ikikamilisha mechi za Kundi A kwa kuvaana na Jang’ombe Boys jioni ya jana Jumatatu kuwania kucheza nusu fainali na usiku Taifa Jang’ombe na watetezi ya Kombe hilop URA ya Uganda walikuwa wavaane usiku.

Mkude alisema kuwa Yanga, Azam zote ni timu nzuri, lakini wanachotaka Simba ni kuthibitisha kuwa Simba ni timu bora zaidi yao kama ambavyo walivyozifunika timu hizo katika Ligi Kuu Bara ambayo imesimama ili kuipisha michuano hiyo.