Kwa Kotei Simba wamepata

Monday March 20 2017

By DORIS MALIYAGA

KIPA wa zamani wa Simba na Yanga, Mghana Yaw Berko anamjua vizuri kiungo, James Kotei anayekipiga klabu ya Msimbazi na akasisitiza huyu jamaa ni balaa na Wekundu hao wamepata mchezaji.

Berko amesema, Kotei ambaye ni Mghana mwenzake wanatoka  sehemu moja, pia amecheza naye mpira mtaani ni sawa na mdogo wake hivyo hashangai kusikia mambo mazuri anayoyafanya sasa.

Akizungumza na Mwanaspoti kwa njia ya mtandao kutoka Ghana,  Berko alisema: “Namfahamu Kotei ni kama mdogo wangu, tunatoka sehemu moja na najua vizuri kiwango chake na hata nikisia anavyofanya vizuri huko sishangai.”

“Tangu alipokuwa mdogo anafanya vizuri na kama Simba itampa nafasi na kumwamini kwa kiwango chake najua ataisaidia timu kwa kiasi kikubwa,” alisema Berko ambaye anaujua vizuri mpira wa Tanzania kwa kuwa alicheza kwa misimu kadhaa.

Tangu ajiunge na Simba, Kotei amekuwa na mchango mkubwa ndani ya kikosi kutokana na kufanya vizuri na ameonyesha umahiri kwa kucheza vyema nafasi ya kiungo na beki.

Hata hivyo, ndani ya kikosi cha Simba, Kotei yupo na Mghana mwingine ambaye ni mlinda mlango, Daniel Agyei.