Kumbe Ngoma ni zaidi yao bwana

Friday May 19 2017

By DORIS MALIYAGA

BEKI wa kushoto wa Yanga, Haji Mwinyi Mngwali, bila kificho ametamka kati ya mastraika wote Ligi Kuu mkali wake ni Mzimbabwe, Donaldo Ngoma.

Mngwali ana uzoefu wa misimu miwili kwenye ligi kuu amesema mchezaji huyo ana kila sababu ya kupata pongezi hizo, ana nguvu, akili ya mpira na anajua kufunga.

Akizungumza na Mwanaspoti, Mngwali alisema: “Ni ngumu kumtaja kwa sababu kila mshambuliaji ana ubora wake, lakini kwangu ni Ngoma tu kwa sababu ana sifa zote anazotakiwa kuwa nazo straika mzuri.

“Kwa umbo lake mrefu, ana akili ya mpira, ana nguvu na anajua kufunga sifa ambazo ni washambuliaji wachache huwa nazo, lakini ndiyo hivyo katika kipindi cha hivi karibuni amepatwa na majanga,”alisema Mngwali na kukazia maneno haya, Ngoma hana mpinzani.

Hata hivyo, Ngoma licha ya kuwa msaada mkubwa katika kikosi cha Yanga, ameshindwa kufanya vizuri kutokana na kusumbuliwa na majeruhi ya mara kwa mara.