Kocha amwondoa Manyika Simba

Friday May 19 2017

KIPA wa zamani wa Simba na Taifa Stars, Idd Pazi ameendelea kulilia kipaji cha kipa wa timu hiyo, Manyika Peter Jr, kuwa kinazidi kuporomoka kwa kutoaminiwa na makocha wa klabuni kwake huku wenzake wakipanda juu akiwemo kipa wa Yanga, Beno Kakolanya, ambaye pia alikumbana na changamoto za kusugua benchi.

Tangu msimu huu umeanza, Manyika Jr amedaka mechi moja tu dhidi ya Mbao FC iliyochezwa Uwanja wa Kirumba wakati Beno akidaka mechi sita za ligi kuu na mbili za Kombe la FA.

Akizungumza na Mwanaspoti, Pazi ambaye pia aliwahi kuwakochi makipa wa Simba alisema; “Manyika sasa aondoke Simba, huu siyo muda wa kupoteza kwake, umri haumsubiri yeye, hawezi kupambana kupata nafasi ya kudaka Simba kwani tayari hawamwamini kuwa atafanya mambo makubwa japokuwa ana kipaji kikubwa, Manyika naona anachelewa tu kuendelea kuwepo Simba.

“Anatakiwa kutazama wenzake na kuwa na maamuzi magumu. Hebu angalia kipa wa Yanga huyo Beno alikuwa anakaa benchi lakini akipata nafasi anaonyesha uwezo wa hali ya juu ingawa pia anapaswa kuongeza juhudi ili wakiamua kufanya mabadiliko kwenye nafasi yao basi asipoteze nafasi yake, akikaa nje naye atapotea,” alisema Pazi ambaye ni mnazi wa kutupwa wa Simba.